Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Ruvuma Simoni Maigwa ,akiongea na Wananchi wa Kitongoji cha Dar pori kijiji cha Lunyere, kata ya Mpepo Wilayani Nyasa Mkoani Ruvuma hivi karibuni, Wakati akihamasisha Ulinzi shirikishi katika maeneo ya Mpakani mwa Nchi ya Tanzania na Msumbijiili amani iwepo.picha na (Ofisi ya Mkurugenzi Mtendaji Wilaya ya Nyasa)
************
Wananchi wa Kata ya Mpepo Wilayani Nyasa, wamempongeza Kamanda wa Jeshi la polisi Mkoa wa Ruvuma Simon Maigwa, kwa kuwakikishia usalama wa mali na maisha licha ya kuishi Karibu na mpaka wa Tanzania na Msumbiji.
Wananchi hao, wametoa pongezi kwa kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoani Ruvuma,
katika Mkutano wa Hadhara uliofanyika katika Kijiji cha Lunyele kata ya Mpepo Wilayani Nyasa hivi karibuni. Mkutano aliokuwa na lengo la kuimarisha ulinzi shirikishi katika eneo la mpakani mwa Nchi ya Tanzania na Msumbiji.
Wananchi hao walifafanua kuwa awali, kulikuwa na matukio yaliyokuwa yakiwapa hofu ya kufanya kazi zao, kwa kuwa ilikuwa haiwezekani kwenda hata kulima shambani, lakini mara baada ya kuimarisha Ulinzi na Usalama, sasa wanafanya kazi zao kwa amani, na kumtaka Kamanda huyo kuwapa kibali cha kujenga kituo cha Polisi katika Tarafa ya Mpepo ili kuweza kukabiliana na matukio ya kihalifu katika Tarafa ya Mpepo kwa kuwa ni tarafa inayopakana na Nchi jirani Ya Msumbiji.
Wananchi hao waliongeza kuwa wana imani na kamanda huyo, kwa kuwa tukio
linapotokea huwa anakuja mwenyewe, bila kutuma mwakilishi na hata leo katika
mkutano wa kuimarisha ulinzi shirikishi na usalama wewe mwenyewe umekuja.
“Kamanda wa Polisi sisi tuna imani kubwa sana na wewe kwa kuwa kila mara
umekuwa pamoja na sisi bila kutuma mwakilishi unafika wewe mwenyewe. sisi sote uliyozungumza tumeyaelewa na tutayafanyia kazi na tunakupongeza sana kwa juhudi zako za ufanyaji kazi wako alisema Kiliani Kumburu huku akishangiliwa na wananchi wengine” .
Kamanda wa jeshi la Polisi Mkoa wa Ruvuma simon Maigwa, Akiongea na wananchi hao katika mkutano huo wa hadhara, aliwahakikishia Usalama wa mali na maisha yao, na kuwataka wafanye kazi za kujenga taifa bila woga wowote kwa kuwa mkoa wa Ruvuma ni salama na hakuna tatizo lolote na atakayeingia kwa kujaribu kuhatarisha Usalama kamwe hataweza,na hatatoka salama.
Aliongeza kuwa kuhusu ombi la ujenzi wa kituo cha polisi cha kisasa kitakachohudumia Tarafa ya Mpepo Wilayani hapa, amelipokea na hana pingamizi lolote na atashirikiana nao kwa hali na mali katika kutatua changamoto za ujenzi huo, na atawaletea polisi na vifaa kwa ajili ya kuhakikisha jamii inakuwa salama muda wote na wanafanya kazi bila uoga wowote.
“Napenda kuwaeleza ndugu wananchi wa kata hii ya Mpepo kuwa Ruvuma ni salama kila mtu aendelee kufanya shughuli zake za kujiletea maendeleo,yeyote atakayejaribu kuingia na kujaribu kutishia amani wananchi kamwe, hatatoka salama. Na nimesikia mnahitaji kujenga kituo cha Polisi hakuna tatizo tushirikiane tujenge na mimi nitaleta Askari mara baada ya kujenga kituo cha kisasa cha polisi kataka kijiji cha tingi ambapo ni makao makuu ya Tarafa ya Mpepo”alisema kamanda Maigwa.
Aliongeza kuwa katika kila Kata ameleta polisi Kata ambaye anatakiwa Kuishi katika kata husika na kuhakikisha ulinzi na Usalama unaimarika kila kata.Hivyo aliwataka wamnanchi hao kushirikiana na Polisi kata aliyeletwa.
Aidha katika hatua nyingine aliendesha harambee ya kuchangia ujenzi wa kituo cha Polisi, cha Tarafa ya Mpepo ambapo jumla ya shilingi laki mbili na ishirini na nne elfu (224,000/=) zilipatikana na kukabidhiwa kwa Ofisa Tarafa wa Tarafa ya Mpepo.
Naye Mkuu wa wilaya ya Nyasa Isabela Chilumba ambaye pia ni mwenyekiti wa kamati ya ulinzi na usalama katika Wilaya hii aliwataka wananchi kuhamasika na kujitoa kwa dhati kuchangia ujenzi wa kituo hicho cha polisi kwa kila kaya kuchangia nguvu zao kwa kuwa, ulinzi ni muhimu sana katika jamii . kwa sasa kituo kilichokuwepo ni kidogo ambacho hakina uwezo wa kuhudumia Tarafa yote ya Mpepo.
Pia aliwataka viongozi wa serikali ya vitongoji, Kijiji, na Kata zote kuwa na Daftari la kusajli wageni wote wanaoingia ili kuweza kujua ni wahalifu au ni raia wema.