***********
NA MWAMVUA MWINYI,KIBAHA
HALMASHAURI ya Mji wa Kibaha,mkoani Pwani, imejiwekea mkakati wa kuwa na dampo la kisasa ,litakalokidhi vigezo ikiwemo kutokuwa na madhara hasi kwa wananchi, huko eneo la Misugusugu ambapo litagharimu kiasi cha sh.bilioni Tatu.
Dampo lililopo sasa lipo Mitamba ambalo linaelezwa linahemewa hivyo kwa mkakati huo italeta ahueni kwa dampo hilo,miaka ijayo.
Akielezea mpango huo, ofisa mahusiano,habari na mawasiliano ,halmashauri ya Mji wa Kibaha, Innocent Byarugaba alisema gharama zinazokadiriwa ni bilioni Tatu lakini halmashauri ikiweka fedha hiyo itashindwa kujiendesha .
Aidha, alieleza juhudi za kuandika maandiko sehemu mbalimbali zinafanyika ili kupata wafadhili.
Byarugaba alisema kwamba, halmashauri imeshatenga milioni 10.2 kwa ajili ya kuandaa barabara ya kuelekea katika dampo kwa kiwango cha changalawe, kutokea barabara kuu kutokana na barabara hiyo kuharibika.
“TARURA nayo imetenga milioni 30 kwa mwaka wa fedha 2019-2020 ili kuboresha barabara hiyo iweze kupitika kirahisi”alielezea ofisa habari huyo.
Ofisa mawasiliano huyo alifafanua,kwa sasa vipo pia vikundi vilivyosajiliwa katika kata mbalimbali ambavyo vinapita kukusanya taka kwenye kaya na kulipwa tozo kidogo.
Byarugaba alibainisha, kwa sasa halmashauri haina kampuni yoyote ya kuzoa taka hivyo amewatahadhalisha wananchi kuwa chonjo na watu matapeli watakaodai wapo kwenye kampuni inayotambulika na halmashauri na kukusanya taka.
Nae diwani wa kata ya Tumbi, Hemed Chanyika alisema kampuni ya kuzoa taka bado ni tatizo kwani kampuni iliyokuwepo awali imesimamishwa zaidi ya miezi mitatu .
Aliwataka wakazi wa kata ya Tumbi ,kuendelea na utaratibu wa kuchimba mashimo kuhifadhi taka na kuzichoma badala ya kulundika uchafu kwenye mifuko kusubiria wakusanyaji taka.