*Wazungumzia namna ya kuimairisha ushirikiano baina ya nchi hizo mbili WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amekutana na kufanya mazungumzo na Rais wa Misri Abdel Fattah Al- Sisi, ambapo wametumia fursa hiyo kuzungumzia masuala mbalimbali ikiwemo namna ya kuimarisha ushirikiano baina ya nchi za Tanzania na Misri.Mbali na kuzungumzia masuala hayo ya kuimarisha ushirikiano katika nyanja mbalimbali zikiwemo za kisiasa, kiuchumi na kijamii, pia Waziri Mkuu amemfikishia Rais wa Misri salamu kutoka kwa Rais wa Tanzania Dkt. John Magufuli.Mazungumzo baina ya Waziri Mkuu na Rais wa Misri yamefanyika leo (Jumatano, Juni 10, 2019) Ikulu jiji Cairo, ikiwa ni katika siku ya tatu na ya mwisho ya ziara yake ya kikazi nchini Misri. Katika ziara hiyo ameambatana na Waziri wa Kilimo, Japhet Hasunga.Waziri Mkuu amemaliza ziara yake ya kikazi nchini Misri ambapo katika uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Cairo ameagwa na Waziri wa Kilimo na Uhaulishaji wa Ardhi wa Misri, Dkt. Ezz Eldien Abo Setit.Akiwa ziarani nchini Misri, Waziri Mkuu alikutana na kufanya mazungumzo na Waziri Mkuu wa Misri, Dkt. Mostafa Madbouly katika siku yake ya kwanza ya ziara yake, ambapo aliwakaribisha wawekezaji na wafanyabiashara kutoka Misri waje kuwekeza nchini.Pia, Waziri Mkuu alitembelea miradi mbalimbali ya maendeleo nchini humo ambayo ni pamoja na mradi wa ujenzi wa makao makuu mapya ya nchi hiyo, mradi wa awamu ya pili ya upanuzi wa mfereji wa Suez Canal na kiwanda kikubwa cha ngozi.
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, akizungumza na Rais wa Jamhuri ya Kiarabu ya Misri, Abdel Fatah Al Sisi, katika Ikulu ya Rais, mjini Cairo, Julai 10.2019. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu).
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, akipeana mkono na Rais wa Jamhuri ya Kiarabu ya Misri, Abdel Fatah Al Sisi, katika Ikulu ya Rais, mjini Cairo, Julai 10.2019. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
……………………..