Kaimu Mkurugenzi wa Uchunguzi TAKUKURU, Bw.Ali Mfuru akiongea na wanahabari katika Ukumbi wa mkutano wa taasisis hiyo Jijini Dar es Salaam.
Kaimu Mkurugenzi wa Uchunguzi TAKUKURU, Bw.Ali Mfuru akiwa na Mtuhumiwa Bw.Omary Khamis Chuma baada ya kukamatwa kwa tuhuma za kujifanya Afisa Serikali kutoka Ofisi za Usalama wa Taifa.
********************
NA EMMANUEL MBATILO
Maafisa wa taasisi ya kuzuia nakupambana na Rushwa (TAKUKURU) wamemkamata Bw.Omary Khamis Chuma (55) kwa tuhuma zakujifanya Afisa wa Serikali kutoka ofisi ya Usalama wa Taifa akitaka kumtapeli Mkuu wa Wilaya ya Kisarawe, Mh.Jokate Mwengelo.
Mtuhumiwa huyo ambaye ni mkazi wa Chamanzi Wilaya ya Temeke jijini Dar es Salaam, alifika katika ofisi za Mkuu wa Wilaya ya Kisarawe Mh.Jokate Mwengelo kwa nia ya kumtapeli kwa kujifanya kuwa yeye ni Afisa wa Serikali kutoka Usalama wa Taifa.
Akizungumza na Wanahabari jijini Dar es Salaam, Kaimu Mkurugenzi wa Uchunguzi TAKUKURU, Bw.Ali Mfuru amesema kuwa baada ya kupokea taarifa hizo pamoja na taarifa kutoka katika vyanzo mbalimbali, taasisi hiyo ilianzisha uchunguzi dhidi ya mtuhumiwa huyo Na.100 (b) cha Sheria ya kanuni ya adhabu (Penal Code) Sura ya 16 marejeo ya mwaka 2002.
“Hatua ya kumkamata tapeli huyu imefikiwa takribani wiki tatu tu tangu TAKUKURU iutangazie Umma juu ya kukamatwa kwa matapeli wengine sita waliokuwa wakishiriki kufanya utapeli”. Amesema Bw.Mfuru.
Aidha, Bw.Mfuru ametoa agizo kwa kuwataka matapeli kuacha mchezo huo kwani TAKUKURU iko macho na inayo Mamlaka kisheria ya kuwachukulia hatua wale wote wanaojihusisha na vitendo vya utapeli.
Vilevile Bw.Mfuru amesema wataendelea kuhimiza wananchi kuwapatia taarifa sahihi za matapeli wa aina hiyo au yeyote anayejihusisha na vitendo vya Rushwa ili hatua stahiki ziweze kuchukuliwa bila kumwonea mtu au kumpendelea yeyote.