Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) imepatiwa msaada wa machine ya kisasa ya Optical Coherence Tomography (OCT) ya kusaidia kupima magonjwa ya macho yenye zaidi ya thamani ya Shilingi milioni 100.
Msaada umetolewa na Shule ya Kwaya ya Westminister Cathedral ya nchini Uingereza kupitia Hospitali ya Mtakatifu Thomas iliyopo nchini humo kwa lengo la kusaidia wagonjwa wenye matatizo ya macho nchini. Mashine ya OCT inatumika kutambua magonjwa yaliopo katika pazia la macho (retina) kwa ajili ya kumsaidia daktari kuamua matibabu sahihi kwa mgonjwa wa macho.
Akizungumza katika shughuli fupi ya kukabidhi mashine ya OCT, mwalimu wa kwaya ya watoto katika Shule ya Kwaya ya Westminister Cathedral nchini Uingereza, Matthew Wright amesema watoto wa kwaya hiyo wenye umri kuanzia miaka minne hadi 13 wametoa msaada ili kusaidia wagonjwa wenye matatizo ya macho nchini.
“Mashine ya OCT itasaidia kutoa matibabu kwa maelfu ya wagonjwa wanaohitaji huduma, huu ni mchango wa watoto wa Shule Kwaya ya Westminister Cathedral ambao wamechanga fedha zao ili kutoa msaada huu,” amesema Mwalimu Wright.
Wright amesema mashine ya OCT pia itasaidia kutoa elimu kwa madaktari zaidi ya 20 wanaosoma jinsi ya kutoa matibabu kwa wagonjwa wanaosumbuliwa na magonjwa ya macho.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Muhimbili, Prof. Lawrence Museru baada ya kupokea msaada amemshukuru Mwalimu Wright pamoja na watoto waliochanga fedha ili kununua machine ya OCT.
Prof. Museru amesema mashine ya OCT itatoa mchango mkubwa kwa wagonjwa wanaosumbuliwa na matatizo ya macho na ameahidi kwamba wataitunza ili iweze kufanya kazi kwa muda mrefu.
Pia, Prof. Museru amewataka wataalam kuhakikisha wanaitumia OCT kwa uangalifu wakati wa kuchukua vipimo kwa wagonjwa ili iweze kuwanufaisha watu wengi zaidi.