Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, ameshiriki katika Mkutano wa 12 wa Dharura wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Umoja wa Afrika kuhusu Mkataba wa Uanzishwaji wa Eneo Huru la Biashara la Afrika (AfCFTA) unaofanyika jijini Niamey nchini Niger.
Makamu wa Rais Mhe. Samia ameipongeza Serikali ya Ghana kwa kuchaguliwa kuwa Makao Makuu ya Sekretarieti ya AfCFTA na kuisihi Kamisheni ya Umoja wa Afrika kuharakisha ukamilishaji wa muundo, wa bajeti na mpango kazi wa Sekretarieti hiyo ili ianze kufanya kazi haraka.
Mkutano huo wa Wakuu wa nchi na Serikali umepokea taarifa ya Mheshimiwa Mahamadou Issoufou, Rais wa Jamhuri ya Niger kuhusu utekelezaji wa AfCFTA ambayo imepokelewa na kupishwa na viongozi hao. Mkataba wa Uanzishwaji wa Eneo Huru la Biashara la Afrika (AfCFTA) umeanza kazi rasmi tarehe 30 Mei, 2019 na unahusu uasili wa bidhaa zitakazouzwa katika soko la Afrika, kufungua biashara ya bidhaa kwa asilimia 97 na uanzishwaji wa Sekretarieti ya kusimamia utekelezaji wa Mkataba wa AfCFTA.
Aidha, alimpongeza Mheshimiwa Mahamadou Issoufou, Rais wa Jamhuri ya Niger kwa jitihada zake za kuhakikisha azma ya Umoja wa Afrika ya kuanzisha Soko Huru la pamoja la Afrika inafikiwa. Makamu wa Rais pia alizipongeza nchi 27 wanachama wa Umoja huo zilizoridhia mkataba wa uanzishwaji wa Eneo Huru la Biashara Afrika (AfCFTA) kati ya nchi 54 zilizotia saini mkataba huo na kuahidi kwamba Tanzania itaungana nao baada ya kukamilisha taratibu za ndani.
Kwenye mkutano huo Makamu wa Rais amemuwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli ambapo alitoa salam za Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa Wakuu wa Nchi na Serikali waliohudhuria mkutano huo.
Wakati huo huo Waziri wa Fedha na Uchumi wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar Mhe. Balozi Mohammed Ramia Abdiwawa amesema kwa upande wa Afrika Mashariki Tanzania imepiga hatua zaidi kutokana na kuwepo katika Jumuiya za Afrika Mashariki na SADC, hivyo Tanzania imefaidika sana kutokana na kupanuka kwa Soko hilo.
Nae Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiao wa Afrika Mashariki Dkt. Damas Ndumbaro amesema Tanzania imenufaika na mkutano huo kutokana na kuendelea kujifunza zaidi kuhusiana na Biashara ya pamoja katika Afrika pamoja na kuweza kushiriki kuchagua Muwakilishi wa Bara la Afrika katika nafasi mbalimbali ndani ya Afrika na Duniani kote wakati Tanzania imepata nafasi moja ambapo Bethabina Seja Afisa wa Takukuru amechaguliwa katika Bodi ya kudhibiti Rushwa Barani Afrika.