MBUNGE wa jimbo la Kibaha Mjini ,mkoani Pwani ,Silvestry Koka, amechangia mifuko ya saruji 50 ili kuanza ujenzi wa choo katika shule ya msingi Mwanalugali kutokana na choo kilichopo kuwa kwenye mazingira hatarishi kwa wanafunzi pamoja na sh.milioni 1.5 kwa ajili ya kukarabati darasa shuleni hapo.
Aidha ameitaka jamii ,pamoja na wadau kujenga ushirikiano katika kusaidia kutatua changamoto mbalimbali za sekta ya elimu ili kujenga mazingira bora ya kusomea watoto na hatimae kuinua taalamu zao.
Koka alisema hayo wakati alipokwenda kufungua madarasa mawili ,yaliyokarabatiwa kwa fedha ya halmashauri na kugharimu sh.milioni 25 shule ya msingi Mwanalugali kata ya Tumbi wilayani Kibaha.
“Ninaahidi kutoa msaada wa mifuko ya saruji 50 kwa ajili ya kuanza ujenzi wa choo na milioni 1.5 kukarabati madarasa ambayo miundombinu yake sio mizuri”alielezea Koka.
Hata hivyo ,Koka alisema pia katika sekta ya elimu ameshachangia sh.mil 6 shule ya msingi Boko Timiza,mil.5 shule ya msingi Mkoani ,mil.10 nyumba ya walimu shule ya msingi Mkoani,milioni 8 ujenzi wa vyoo shule ya msingi Kambarage na kusimamia milioni 180 kwa ajili ya mabweni shule ya sekondari Mwanalugali.
Nae diwani wa kata ya Tumbi, Hemed Chanyika alisema,yeye na mbunge walipigania halmashauri na hatimae kutolewa fedha za ukarabati milioni 25 ambazo zimekamilisha ujenzi wa madarasa mawili.
Chanyika,aliahidi kuchangia malori ya mchanga ili kuunga mkono juhudi za wananchi walioanza ujenzi wa choo shuleni hapo.
Awali mwalimu mkuu wa shule ya msingi Mwanalugali, Mariam Mfinanga alisema changamoto kubwa ni upungufu wa matundu ya choo , kuongeza darasa japo moja ili kukidhi mahitaji na ukosefu wa uwanja wa michezo .
Shule hiyo ina jumla ya wanafunzi 271,wavulana 158 na wasichana 113,walimu tisa,shule hiyo ilianza mwaka 2002 ikiwa ni moja ya shule ya Wazazi.