Ofisa Usajili wa Bodi ya Nyama Bw. Geofrey Sosthens akitoa maelezo kwa wananchi waliotembelea katika banda hilo wakati wa maonesho ya Sabasaba ya yanayoendelea barabara ya Kirwa jijini Dar es Salaam.
BODI ya Nyama Tanzania imesema, ifikapo Septemba 30, 2019 ndio itakuwa mwisho kwa wauza nyama mabuchani kutumia magogo na endapo mtu atakaidi atachukuliwa hatua za kisheria kwani magogo hayo yanamadhara kiafya ambayo yanatengeneza mazingira ya kuzaliana kwa wadudu au vimelea vya magonjwa.
Aidha, amesema magogo hayo pia yanasababisha hasara ya upotevu wa nyama, kitaalamu katika kilo 100 inapotea kilo moja, ambapo kwa mwaka muuzaji anapoteza Sh milioni 3.8 ambayo inatosha kununua machine ya kisasa kukatia nyama.
Hayo yalisemwa na Ofisa Usajili kutoka katika bodi hiyo, Geofrey Sosthens wakati wa maonesho ya sabasaba yanayoendelea jijini Dar es Salaam, ambapo aliwata wafanyabiashara wa bidhaa hiyo kutembelea banda lao ili waweze kupata elimu.
Alisema watakao kaidi agizo hilo watachukuliwa hatua na Msajili wa bodi hiyo, kwa sababu tayari amekwisha ziandikia mamlaka za Serikali za Mitaa tangu Februari, mwaka huu kwa maana ya wakurugenzi wa idara zote kuhakikisha wanaboresha maeneo yote yanayizalisha nyama ukiwa pamoja na machinjio, makalo na mabucha.
Ofisa huyo, alisema hawapendi kuyatumia magogo kwa sababu yanamdhara kutokana na kwamba hayasafishiki, ukiwa unakata nyama baada ya mwezi yanakuwa ni mabaki ya muda mrefu, yanatengeneza vimelea vya magongwa ambavyo vinaweza kuleta madhara kwa walaji.
Akizungumzia hasara inayopatikana, alisema mtu akitumia gogo, Kumbuka anatumia na shoka, kinachotokea nyama inagawanyika.
“Kama una bucha inauza kilo 200 kwa siku unaona ni kiasi gani unapoteza, ukipiga hesabu yak kwa mwaka unapoteza sh milioni 3.8 ambayo inatosha kununua mashine ya kisasa ya kukatia nyama, tunawasihi kuacha kuyatumia magogo kwa sababu si salama kwa afya za watumiaji,” alisema Sosthens
Pia, alisema wanahakikisha wanawashauri wamiliki wa mabucha kuhakikisha wanakuwa na mabucha ya viwango ambayo yapo kwenye sheria, viwango hivyo ni pamoja na kuacha kutumia magogo hayo, jambo ambao wamekwisha lisisitiza.
Ofisa alitoa ombi kwa wadau yeyote anayejishughulisha na mnyororo wa thamani wa nyama au anayefanya biashara hiyo au msafirishaji au mfugaji ahakikishe amesajiliwa na kumiliki cheti kutoka katika bodi hiyo.
“Wakijisajili itakuwa rahisi hata kuwaunganisha na masoko, tumepata muitikio mdogo wa wadau kusajiliwa ndiyo maana tunaendelea kutoa elimu, kuhamasisha wadau wote kama sheria inavyowataka,” alisema Sosthens