Waziri Mkuu Mstaafu, mhe.Mizengo Pinda akisaini kitabu cha wageni cha Bodi ya Maziwa wakati akitembelea banda la Wizara ya Mifugo na Uvuvi leo kwenye maonesho ya biashara ya Kimataifa ya 43 yanayoendelea kwenye viwanja vya Mwl.Nyerere barabara ya Kilwa jijini Dar es salaam.
Waziri Mkuu Mstaafu Mhe.Mizengo Pinda akipata maelezo kutoka kwa mkurugenzi msaidizi (uvuvi) Bw.Antony Dadu kuhusu bidhaa zitokanazo na zao la mwani alipotembelea banda la Wizara ya Mifugo na Uvuvi leo kwenye maonesho ya biashara ya kimataifa ya 43 yanayoendelea kwenye viwanja vya Mwl.Nyerere barabara ya Kilwa jijini Dar es salaam.
Waziri Mkuu mstaafu, mhe. Mizengo Pinda, akipata maelezo kutoka kwa Afisa Masoko wa Bodi ya Nyama Tanzania, Bw.Nicholai Chiweka wakati akitembelea banda la Wizara ya Mifugo na Uvuvi kwenye maonesho ya biashara ya kimataifa ya 43 yanayoendelea kwenye viwanja vya Mwl.Nyerere barabara ya Kilwa jijini Dar es salaam.
Na Moses Mwakibolwa
WIZARA ya mifugo na Uvuvi imeendelea kung’ara katika maonesho ya 43 Kimataifa ya Biashara 2019 kwa kunyakua tuzo ya Mifugo na Uvuvi
Akizungumzia ushindi huo Afisa Mifugo mkuu na Mratibu wa Maonesho Kitaifa wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi Mary Yongolo amesema tuzo hiyo imechagiza uwajibikaji katika wizara na kuongeza Moroli ya kazi kwa wafanyakazi wote
Amesema kwa sasa wizara imesogeza huduma karibu zaidi kwa wananchi na kuhakikisha kila mteja anahudumiwa kwa wakati katika mabanda ya sabasaba
Afisa huyo amewataka wadau wa sekta ya Mifugo na uvuvi kufika katika mabanda hayo kupata huduma za haraka kwani maonesho hayo yamekuwa ni fursa kubwa kwa wakazi wa kanda ya mashariki mikoa ya Pwani na Morogoro hasa baada ya serikali kuhamia Dodoma
Aidha amewataka wananchi kutembelea Banda la wizara kuja kujifunza teknolojia mbalimbali za uongezaji thamani wa mazao ya nyama, maziwa na samaki na mbinu ambazo zitawasaidia katika kuboresha bidhaa zao katika masoko
Ameongeza kuwa kutokana na umuhimu mkubwa katika wizara hiyo hivi karibuni wadau watakutana na Dawati la sekta binafsi katika maonesho hayo ambalo ni maalumu katika shughuli zao ikiwa ni pamoja na kuangalia changamoto zinazoikabili sekta pamoja na mikopo kwa wadau
Malengo ya serikali ni kuhakikisha wafugaji wanafuga kibiashara badala ya kufuga kimazoea, hivi karibuni serikali imeongeza kasi katika ujenzi wa viwanda vya nyama na samaki na endapo wadau hawa watawezeshwa basi sekta hii itakuwa kwa kasi kubwa kutokana na rasilimali zilizopo kwenye mifugo na uvuvi
Amekiri kuwa na changamoto katika soko la ndani ambapo amesema ubora wa masoko umekuwa mdogo lakini serikali ya Awamu ya tano inalifanyia kazi na hivi karibuni kutakuwa na masoko ya kiwango cha kimataifa hapa nchini
Kwa upande wa watoa huduma wa nyama amewataka kuja kujifunza njia nzuri ya kuwahudumia wateja kwani awali Changamoto kubwa ilikuwa ni kukata nyama kwa kutumia magogo katika mabucha kitu ambacho kilikuwa si kizuri kwa afya kwa sababu kukatia nyama kwenye gogo kunafyonza uchafu wa majimaji na mifupa midogo ambayo ni hatari kwa afya ya mlaji lakini mpaka hivi sasa wauzaji wa nyama wanatumia mashine za kisasa kukatia nyama kitu ambacho kinaongeza thamani ya bidhaa hiyo sokoni
Amemaliza kwa kusema idadi kubwa ya ng’ombe millioni 30.5 kufikia mwaka 2020 lazima iongeze pato kwa serikali, hivi sasa wizara inaendelea na kazi kubwa ya utoaji elimu kwa wafugaji ambao wengi awali hawakuwa na mwamko wa elimu kitu ambacho kilidumaza soko la bidhaa ya mifugo na kutowasaidia wafugaji kujikwamua kiuchumi
Naye Afisa wa Utafiti wa wizara ya mifugo Neema Urasa amesisitiza umuhimu wa wafugaji kufika kujifunza mambo mbalimbali yaliyopo katika Maonesho hayo kwani wafugaji watakuja kujionea namna bora ya ufugaji wa kisasa
Amesema wafugaji wengi wanafuga kwa mazoea na ukiangalia bidhaa za mifugo zimekosa mvuto sokoni na kushuka kwa thamani ya bidhaa kama ngozi, kwato pamoja na nyama
Ameongeza kuwa hivi sasa kila kitu kwa mifugo kina thamani, ametoa mfano wa damu, ngozi pamoja na nyama yenyewe
Pia siku za hivi karibuni wafugaji wameelewa umuhimu wa kulima nyasi za kisasa kwa ajili ya malisho ya wanyama kitu ambacho kitaongeza thamani ya zao la nyama sokoni
Amemaliza kwa kusema ni vema mifugo ikawa michache lakini yenye ubora sokoni kuliko kuwa na kundi kubwa la mifugo ambalo lina wanyama dhaifu