MKUU wa Mkoa wa Pwani, mhandisi Evarist Ndikilo ametoa miezi mitatu kwa Mkurugenzi wa Halmashauri ya wilaya ya Kisarawe Mussa Gama na Ofisa Utumishi , kuhakikisha idara ya ukaguzi wa ndani inajitosheleza kwa ikama ya watumishi na vitendea kazi.
Ameeleza idara hiyo iangaliwe kwa jicho la tatu, ili iweze kutekeleza majukumu yake kikamilifu wakati wa ukaguzi.
Akizungumza katika baraza maalum la madiwani kupitia hoja za mdhibiti na mkaguzi mkuu wa hesabu za serikali (CAG) ,Ndikilo alieleza baada ya utekelezaji wa agizo hilo ,mkuu wa wilaya hiyo Jokate Mwegelo ampelekee taarifa.
“Kumekuwepo na changamoto ya kiutendaji katika raslimali watu na fedha na kusimamia miradi ya maendeleo”:Hivyo basi wakurugenzi mkoani hapa na watendaji wasimamie ili sheria,kanuni na taratibu zifuatwe kwa lengo la kusaidia mkaguzi akipita kusiwepo na dosari”alifafanua Ndikilo.
Ndikilo aliongezea kwamba, CAG asionekane ni adui kwani ni mshirika wa kuweka mambo vizuri kuhakikisha fedha za serikali haziliwi wala kufujwa.
Nae Mkaguzi wa hesabu wa nje mkoani Pwani, Hamis Juma alitaka ushauri na maoni yaliyotolewa katika hoja 26 zinazoendelea kufanyiwa kazi na halmashauri hiyo zifanyiwe kazi na uhakiki utafanyika 2018/2019.
Awali akimkaribisha mkuu huyo wa mkoa, Mkuu wa wilaya ya Kisarawe Jokate Mwegelo alisema halmashauri hiyo imepokea taarifa ya ukaguzi wa hesabu za mwaka wa fedha 2017/2018 kutoka kwa mdhibiti wa hesabu za serikali mwezi april 2019 ikionyesha hati safi na hoja za ukaguzi.
Nae mkurugenzi wa halmashauri ya Kisarawe ,Mussa Gama alipokea maagizo waliyopatiwa na kudai watahakikisha wanapata hati safi nyingine kipindi kijacho na kuondoa mapungufu yaliyoonekana .
Alibainisha wakati wa ukaguzi imegundua kuwa kitengo cha ukaguzi hakifanyi kazi kwa sababu watumishi wachache watatu badala ya watano na uhaba wa vitendea kazi lakini wameshughulikia na kuongeza mtumishi mmoja na kufikia wanne.