*****************
Felix Mwagara, Mwibara (MOHA)
WAZIRI wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Kangi Lugola amewataka
wakazi wa Jimbo la Mwibara, Wilayani Bunda Mkoa wa Mara,
kuilinda amani iliyopo nchini ili waweze kuendelea kufanya
shughuli zao za kilimo wakiwa na amani.
Lugola ameyasema hayo leo, katika Kata ya Butimba, jimboni
kwake, alipokuwa anazungumza na wananchi wa Kijiji cha
Mwiseni, mara baada ya kushiriki shughuli za mazishi ya mtoto
wa dada yake katika Kijiji hicho, aliyefariki hivi wiki hii mkoani
Mwanza.
Lugola alisema Tanzania ina amani kwasababu inautamaduni wa
kuwa na amani, hivyo asitokee mtu akaharibu utamaduni huo
ambao nchi inaendelea kuhudumisha.
“Ndugu zangu wana Mwiseni, Wana Mwibara, amani tulionalo
ndiyo inatuwezesha leo tunalima vizuri, tunavua samaki, leo
tunakula vizuri, leo tunafanya shughuli mbalimbali za maendeleo,
hivyo tuendelee kuitunza amani hii,” alisema Lugola.
Aliongeza kuwa, Wizara yake kupitia Jeshi la Polisi ipo imara,
Serikali ya Rais Dkt. John Magufuli ipo imara na inaendelea
kuwalinda Watanzania mahali popote walipo nchini, na hakuna
mtu atakaye ivunja amani hiyo.
Aidha, Lugola aliwataka wananchi hao kuhifadhi vyakula vizuri ili
kuepusha janga la njaa kwa hapo baadaye na kusababisha
wananchi kuja kuteseka kwa ukosefu wa vyakula na kusababisha
mateso katika familia.
“Tutunzeni vyakula vyetu, msitumie hovyo, kuweni makini na
matumizi ya vyakula, sitaki nije kuona mnateseka na njaa,
hakikisheni mnatunza vyakula kwa ajili ya matumizi ya baadaye,
ogopeni njaa kama ukoma,” alisema Lugola.
Lugola ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo hilo, alifanya ukaguzi wa
miradi ya maendeleo akikagua madarasa ya shule ya msingi
pamoja na zahanati.
“Nataka hili darasa likamilike kwa wakati, natoa mifuko ya saruji
100 ili kuikalimisha zahanati hii katika Kata hii, na pia nitaleta
mabati ili maendeleo yazidi kuwafikia wananchi wa jimbo hili,”
alisema Lugola.
Waziri Lugola ameanza ziara yake leo, ambapo anatarajia kufanya
ziara hiyo katika vijiji vya Kata zote jimboni humo.