Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Maendeleo ya biashara Tanzania (TANTRADE), Bw.Edwin Rutageruka akizungumza na Wafanyabiashara, Wakulima na Wanunuzi mbalimbali walioweza kufika katika ufunguzi wa Mikutano ya biashara Sekta ya Matunda na Mbogamboga katika maonesho ya biashara yanayoendelea katika viwanja vya Mwalimu Nyerere barabara ya Kilwa Jijini Dar es Salaam.
Wafanyabiashara, Wakulima na Wanunuzi mbalimbali wakifuatilia mjadala uliopo katika ufunguzi wa Mikutano ya biashara Sekta ya Matunda na Mbogamboga katika maonesho ya biashara yanayoendelea katika viwanja vya Mwalimu Nyerere barabara ya Kilwa Jijini Dar es Salaam.
*************
NA EMMANUEL MBATILO
Mamlaka ya Maendeleo ya biashara Tanzania (TANTRADE) imewataka wakulima pamoja na wafanyabiashara nchini kushirikiana nao ili kuweza kutatua changamoto ambazo wanakutana nazo katika shughuli zao.
Ameyasema hayo leo Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Maendeleo ya biashara Tanzania (TANTRADE), Bw.Edwin Rutageruka katika ufunguzi wa Mikutano ya biashara Sekta ya Matunda na Mbogamboga katika maonesho ya biashara yanayoendelea katika viwanja vya Mwalimu Nyerere barabara ya Kilwa Jijini Dar es Salaam.
Akizungumza na wadau mbalimbali Bw. Rutegeruka amesema kuwa pamoja na mikakati ya Mamlaka hiyo na wadau wengine ya kuendeleza bidhaa za Tanzania, yawapasa kutoa ushirikiano wa kutosha ili kutambulisha uwezo wa ubora wa kampuni katika kufanya biashara ili kutambulisha uwezo na ubora wa kampuni katika kufanya biashara ili waunganishe na fursa ambazo wanazipata.
Aidha, Bw.Rutageruka amesema kuwa takwimu zinaonyesha kuwa thamani ya mauzo ya bidhaa za viwandani iliongezeka na kufikia dola za Marekani milioni 794.6 mwaka 2018 kutoka dola milioni 693.7 mwaka 2017, sawa na ongezeko la asilimia 14.5
“Takwimu zinaonyesha kuwa Tanzania ina takribani viwanda 49,243 ambavyo kati yake, 393 ni viwanda vikubwa vilivyopata usajili mwaka 2016/2017. Viwanda hivyo vilivyosajiliwa miongoni wao ni viwanda vinavyozalisha bidhaa mbalimbali ikiwemo usindikaji wa matunda na mbogamboga lakini bado vinakabiliwa na changamoto ya ukosefu wa malighafikutokana na upungufu wa uzalishaji wa ubora wa matunda,mboga, maua na viungo”. Amesema Bw.Rutageruka.
Pamoja na hayo, Bw. Rutageruka amemalizia kwa kusema kuwa nchi yetu iko katika mwaka wa tatu wa utekelezaji wa mpango wa pili wa maendeleo wa miaka mitano wa mwaka 2016/2017-2020/2021, unaolenga kujenga uchumi wa viwanda ili kuchochea mageuzi ya kiuchumi na maendeleo ya Watanzania.