Home Mchanganyiko TANZANIA NI MIONGONI MWA NCHI AMBAZO ZINAENDELEA KUFANYA VIZURI KATIKA KUPAMBANA NA...

TANZANIA NI MIONGONI MWA NCHI AMBAZO ZINAENDELEA KUFANYA VIZURI KATIKA KUPAMBANA NA RUSHWA

0
***********************
NA EMMANUEL MBATILO
Tafiti zinaonyesha kuwa Tanzania imeanza kufanya vizuri katika mapambano dhidi ya Rushwa na Utawala Bora katika kipindi hiki cha hivi karibuni na kuendelea.
 Tafiti hizo zimefanywa na taasisi za ndani na nje ya nchi zimeonyesha kuwa Tanzania imeanza kufanya vizuri katika mapambano dhidi ya Rushwa huku ikiimarisha utawala bora.
Hayo yalisemwa jana na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma Mh.George Mkuchika, wakati wa Kongamano la siku maalumu dhidi ya Rushwa katika maonyesho ya 43 ya Kimataifa ya Biashara yanayofanyika Dar es Salaam (DITF).
Mh. Mkuchika amesema serikali inatumia nguvu kubwa kupambana na Rushwa ili kuiletea maendeleo nchi na kutekeleza Ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM).
“Mipango yote ya serikali ya kuifikisha nchi katika uchumi wa kati kupitia sekta ya Viwanda hauwezi kufikiwa pasipo na mapambano dhidi ya Rushwa ndiyo maana tumekuwa wakali sana, ili kuwe na mapambano ya rushwa lazima kuwepo na utashi wa kisiasa,” amesema Mh.Mkuchika.
Aidha Mh. Mkuchika amesema kuwa matokeo ya mapambano hayo ni kuongezeka kwa wigo wa upatikanaji wa huduma kwa Watanzania ikiwemo Elimu bure.
Naye Mkurugenzi Mkuu wa TANTRADE Edwin Lutageruka, alisema Rushwa imekuwa kikwazo kikubwa cha uwekezaji kwani wengi wanakata tamaa na kuondoka kutokana na kushindwa kuhimili milolongo.
Bw.Edwin lutageruka amesema kuwa wawekezaji wengi wanahofia kupoteza muda mwingi wa ufuatiliaji, matumizi makubwa ya rasilimali fedha hatimaye kumaliza mitaji.Milolongo ya rushwa kwa wawekezaji ndiyo sababu ya wananchi kukosa huduma ya bidhaa bora na kusababisha uingizwaji wa bidhaa kwa njia zisizo rasmi.
Kwa upande wake Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Dk. Bashiru Ally, alisema Ilani ya CCM iliweka lengo la kukabili mambo manne ikiwemo ajira, umasikini, rushwa na ufisadi pamoja na  usalama na amani ya nchi ndiyo maana kumekuwa na upungufu wa matukio ya rushwa nchini.