Mafundi wakiendelea kufunga mashine mpya ya kisasa ya hospitali ya rufaa ya Haydom Mkoani Manyara, wakiendelea kushoto ni Mkurugenzi wa hospitaki hiyo Dkt Emmanuel Nuwass.
*************
HOSPITALI ya rufaa ya Haydom Wilayani Mbulu, Mkoani Manyara imenunua mashine mpya ya kisasa ya uchunguzi (X-ray) kwa lengo la kuhudumia wagonjwa wengi, kuongeza ufanisi na kutoa huduma kwa urahisi zaidi.
Hospitali hiyo inahudumia wagonjwa wa zaidi ya mikoa sita nchini, ikiwemo Manyara, Singida, Dodoma, Tabora, Arusha na Simiyu ambapo kifaa hicho kitaongeza mikakati ya kupandishwa hadhi kuwa hospitali ya kanda.
Mkurugenzi wa hospitali ya Haydom Dk Emmanuel Nuwass alisema mashine hiyo mpya ya kisasa ya kidigital imenunuliwa kwa gharama ya sh300 milioni.
Dk Nuwass alisema mashine hiyo ya kisasa kutoka Ufaransa itasababisha ufanisi mkubwa katika utendaji kazi wake katika kuwahudumia wagonjwa wa hospitali hiyo tofauti na awali.
Alisema mashine hiyo ina uwezo mkubwa wa kupiga picha kwa ubora na muda mfupi tofauti na ile iliyokuwa inatumika kwa teknolojia ambayo imepitwa na wakati.
“Mashine hii ni ya kisasa na ya kipekee kwani kwa hapa nchini zipo mbili za toleo hili katika hospitali ya Haydom na hospitali ya Bugando jijini Mwanza,” alisema Dk Nuwass.
Alisema mashine hiyo ya kisasa ya mionzi zaidi ya kuhudumia watu wengi kwa muda mfupi, ubora wa picha zake utasababisha tatizo la mgonjwa kuonekana kwa urahisi.
Alisema pamoja na kutoa huduma kwa wagonjwa pia mashine hiyo itaongeza mikakati yao ya kufanikisha hospitali hiyo kupandishwa hadhi kutoka ya rufaa hadi kuwa ya kanda.
Hata hivyo, mmoja kati ya wakazi wa eneo hilo, John Matle aliyekuwa hospitalini hapo alipongeza jitihada za Dk Nuwass katika kuboresha miundombinu ya hospitali ya Haydom.
“Ile mikakati ya kuhakikisha hospitali ya rufaa ya Haydom inakuwa ya kanda inaweza ikafanyika kutokana na mikakati na mipango bora kama hii inayofanywa na Dk Nuwass,” alisema Matle.