Mbunge wa Jimbo la Simanjiro Mkoani Manyara, James Ole Millya (kushoto) akiwa na wachina, maofisa wa madini na polisi wakikagua eneo la uwekezaji wa madini ya ulanga Mji mdogo wa Mirerani.
Mbunge wa jimbo la Simanjiro Mkoani Manyara, James Ole Millya (kulia) akiwaonyesha wawekezaji wa China eneo mojawapo yanapopatikana madini ya ulanga Mji mdogo wa Mirerani.
Mbunge wa jimbo la Simanjiro Mkoano Manyara, James Ole Millya (kulia) akiwasikiliza wawekezaji raia wa China kwenye eneo la madini ya ulanga Mji mdogo wa Mirerani.
………………….
RAIA tisa wawekezaji wa China wanatarajia kuwekeza kwenye uchimbaji mkubwa wa madini ya Grafite (ulanga) Mji mdogo wa Mirerani Wilayani Simanjiro Mkoani Manyara.
Madini hayo ya ulanga hutumika kwa ajili matengenezo ya vitu mbalimbali ikiwemo betri za simu, betri za kurunzi, kalamu ya risasi na mengineyo.
Mbunge wa jimbo la Simanjiro, James Ole Millya, alisema wawekezaji hao wanatarajia kufanya uwekezaji mkubwa wa madini hayo ya viwandani katika eneo hilo.
Ole Millya alisema uwekezaji huo utawanufaisha watanzania wengi hususan wa wilaya ya Simanjiro ikiwemo kuwapatia ajira za kudumu na za muda mfupi.
Alisema awali wawekezaji hao walifika kwenye nchi ya Msumbiji na kukagua eneo la kuchimba madini hayo ya ulanga ndipo wakaja Tanzania kwa lengo la kukagua na kuwekeza.
“Ninatarajia serikali itatoa ushirikiano mkubwa wa kutosha ili wawekezaji hao wafanikishe kuanzisha viwanda vikubwa katika uchimbaji wa madini hayo ya ulanga,” alisema Ole Millya.
Hata hivyo, mkuu wa wilaya ya Simanjiro, Zephania Chaula alisema serikali itawapa ushirikiano mkubwa wawekezaji hao na kuwaandalia mazingira rafiki ya kuwekeza viwanda katika uchimbaji wa madini hayo.
“Tunampongeza mbunge wetu kwa kufanikisha upatikanaji wa wawekezaji hao ambao kwa kiasi kikubwa watazalisha ajira kwa wana Simanjiro kupitia viwanda na kulipa kodi serikali,” alisema Chaula.
Ofisa madini mkazi wa Mirerani, Daudi Ntalima alisema wametoa ushirikiano kwa wawekezaji hao ambao walikagua maeneo yote wanayotaka kuwekeza katika sekta hiyo.
“Maofisa wangu wametembea mguu kwa mguu na wawekezaji hao ili kuhakikisha wanapata nafasi ya kufanya ukaguzi kabla ya kuwekeza pindi sheria, taratibu na kanuni zikifuatwa,” alisema Ntalima.
Wilaya ya Simanjiro ina utajiri mkubwa wa aina mbalimbali ya madini zaidi ya 150 ikiwemo Tanzanite, Ruby, Green Tourmarine, Green Ginet, Saphure, Rose na mengineyo.