*******
Na Mwandishi wetu Mihambwe
Afisa Tarafa Mihambwe *Emmanuel Shilatu* amefanya ziara ya kukagua ujenzi wa miradi ya umaliziwaji wa maboma kwa shule za msingi ambazo Serikali imetoa fedha kwa ajili ya ukamilishwaji wake yaliyopo kata za Miuta, Mkoreha na Michenjele.
Kwenye ziara hiyo Gavana Shilatu ametoa maelekezo kwa kamati za ujenzi ya miradi hiyo wahakikishe inamalizwa kwa wakati na kwa ubora tayari kutumiwa na Wanafunzi.
*”Nawapongeza Wanakijiji kuanzisha miradi hii na tunamshukuru Rais Magufuli kutoa fedha za kumalizia maboma haya. Nawapa maagizo uongozi wa shule na kamati ya ujenzi muhakikishe ndani ya wiki mbili kuanzia sasa miradi hii inamalizwa kwa wakati na ubora unaolingana na thamani ya fedha iliyotolewa na Serikali. Nami mara kwa mara nitakuwa napita pita kukagua maendeleo ya ujenzi.”* Alisisitiza Gavana Shilatu.
Serikali ya awamu ya 5 inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania *Dkt John Magufuli* kupitia mradi wa lipa kulingana na matokeo imetoa fedha Tsh. Milioni 42.5 kukamilisha maboma ya madarasa 3 na uwekaji wa Madawati yake kwa shule za Msingi Ngongolo, Shule ya Msingi Misufini na Shule ya Msingi Mmalala yaliyopo Tarafa ya Mihambwe.