Washiriki wa mchezo wa mpira wa Kengele na mabingwa wapya timu ya mpira wa kengele kutoka mkoa wa Tabora wasichana wakiwa katika mchezo wa fainali dhidi ya Morogoro ambapo matokeo Tabora 16- 7
Baadhi ya wachezaji wa soka maalum wakipambana vikali kuingia hatua ya nusu fainali baina ya timu za mikoa ya Dodoma na Simiyu.
…………………………..
Na Mathew Kwembe, Mtwara
Timu ya wavulana kutoka mkoa wa Dar es salaam na timu ya wasichana kutoka mkoa wa Tabora zimefanikiwa kujishindia nafasi ya kwanza baada ya kufanikiwa kuwabwaga wapinzani wao katika kuwania ubingwa wa mpira wa kengele katika fainali za UMITASHUMTA zilizofanyika jana kwenye viwanja vya chuo cha ualimu Mtwara.
Timu ya wavulana kutoka mkoa wa Dar es salaam ndiyo ilikuwa ya kwanza kufanikiwa kutwaa taji hilo baada ya kuifunga timu ya mkoa wa Lindi 23-13, huku mshindi wa tatu kwa upande wa wavulana ilikuwa timu ya Tanga baada ya kuifunga Tabora 14-7.
Kwa wasichana Tabora ilishika nafasi ya kwanza baada ya kuilaza Morogoro 16-7 na mshindi wa tatu kwa wasichana ilikuwa timu kutoka mkoa wa Arusha baada ya kuilaza Tanga 8-6.
Wakati huo huo matokeo ya mchezo wa robo fainali soka wasichana baina ya Mwanza na Dar es salaam matokeo ni kuwa timu ya Mwanza ilifanikiwa kuingia nusu fainali baada ya kuifunga Dar es salaam kwa kutumia mikwaju ya penati 3-2 baada ya kutoka sare ya goli 1-1, Manyara ilifungwa na Mara 0-1, Kagera iliitoa Simiyu kwa penati 4-1 baada ya kutoka suluhu ya bila kufungana, na Morogoro iliondolewa na Kilimanjaro kwa penati 5-6 baada ya kutoka suluhu ya bila kufungana.
Katika soka maalum timu ya mkoa wa Dodoma ilifanikiwa kuilaza Kilimanjaro 1-0, Tabora ilichapwa na Ruvuma 0-5, Mtwara iliifunga Kagera 2-0, na Dar es salaam ilichabangwa na Shinyanga 1-5.
Kufuatia matokeo hayo, timu zilizofuzu hatua ya nusu fainali kwa soka wasichana ni Mwanza ambayo itacheza na Mara, huku mchezo mwingine utahusisha Kagera watakaomenyana na Kilimanjaro.
Katika soka maalum wavulana michezo ya nusu fainali itahusisha Dodoma watakaopambana na Ruvuma na mchezo mwingine utahusisha timu za Mtwara itakayopambana na Shinyanga
Kwa upande wa soka wavulana timu za Dar es salaam, Manyara, Mwanza, Geita, Kagera na Tanga tayari zimefuzu hatua ya robo fainali na zinasubiri wapinzani wao wacheze ili waweze kujua timu zitakazoshindana nazo.
Katika matokeo ya mechi zilizochezwa jana Iringa ilibugizwa na Lindi 1-7, Mbeya ilifungwa na Pwani 0-1, Mwanza iliichapa Simiyu 6-1, katavi ilifungwa na Songwe 2-4, Kagera ilifungwa na Rukwa 0-1 na Arusha iligalagazwa na Tabora kwa magoli 0-9.