**********
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema kaya zinazoishi kwenye makazi bora zimeongezeka kwa asilimia 16 katika kipindi cha miaka sita ikilinganishwa na hali ilivyokuwa mwaka 2011/2012.
“Kaya zinazoishi kwenye nyumba zenye paa la kisasa zilizoezekwa kwa bati zimeongezeka kutoka asilimia 68 mwaka 2011/2012 hadi kufikia asilimia 84 mwaka 2017/2018 wakati kuta za kudumu zimeongezeka kutoka asilimia 46 mwaka 2011/2012 hadi kufikia asilimia 79 mwaka 2017/2018,” amesema.
Ametoa kauli hiyo leo jioni (Jumamosi, Juni 29, 2019) wakati akizungumza na viongozi na wananchi mara baada ya kuzindua Jengo la Ofisi ya Taifa ya Takwimu lililoko Makulu, Manispaa ya Jiji la Dodoma.
Waziri Mkuu ambaye alimwakilisha Dkt. John Pombe Magufuli, pia alizindua ripoti ya matokeo ya viashiria muhimu vya utafiti wa mapato na matumizi ya kaya binafsi Tanzania Bara ya mwaka 2017/18.
Waziri Mkuu alisema takwimu hizo ni matokeo ya utafiti uliofanywa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu na zinaonyesha jitihada za Serikali ya Awamu ya Tano za kujenga Tanzania ya Viwanda zinaendelea kuwanufaisha wananchi kwa zinagusa moja kwa moja katika sekta ya ujenzi kama vile viwanda vya saruji, mabati, nondo, na vinginevyo.
Waziri Mkuu alisema lengo la Serikali ni kuona kila Mtanzania anaishi kwenye makazi bora kwani makazi bora huimarisha afya za wakazi na afya bora ni mtaji wa msingi kwa kila mwanadamu kwa kufanya kazi na hivyo kukuza uchumi.
“Tuendelee kuunga mkono jitihada za Serikali kuhamasisha wawekezaji wa ndani na nje waje wawekeze kwenye viwanda vya saruji, mabati, na marumaru ili kuongeza uzalishaji na kuleta ushindani wa bei ambao utawanufaisha watu wengi na kuwapatia fursa za kujenga makazi bora ya kuishi,” alisema.
Waziri Mkuu alisema mbali na makazi bora, utafiti huo umebainisha uwepo wa ongezeko la kaya zilizounganishwa kwenye umeme wa Gridi ya Taifa kutoka asilimia 18 mwaka 2011/2012 hadi kufikia asilimia 29.1 mwaka 2017/2018. “Jitihada za Serikali chini ya Mpango wa Umeme Vijijini (REA), zinaendelea na utekelezaji wa Mradi Kabambe wa Awamu ya Tatu wa kusambaza nishati vijijini unaojumuisha vijiji 7,873 katika wilaya na mikoa yote ya Tanzania Bara ambao unatekelezwa kwa kipindi cha miaka mitano ulioanza mwaka wa fedha 2016/17 na unategemewa kukamilika mwaka 2020/2021,” alisema.
Akizungumzia hali ya umaskini barani Afrika, Waziri Mkuu alisema kiwango cha umaskini wa kipato cha Watanzania hakitofautiani sana na nchi nyingine ndani ya bara hilo. “Tukiangalia hali ya umaskini katika nchi nyingine za Bara la Afrika kwa miaka ya hivi karibuni, nikianza na Kenya kiwango cha umaskini wa mahitaji ya msingi ni asilimia 36.8 (mwaka 2015), Afrika ya Kusini asilimia 55.5 (mwaka 2015), Rwanda asilimia 38.2 (mwaka 2016), Zambia asilimia 54.4 (mwaka 2015), Ethiopia asilimia 23.5 (mwaka 2015) na Zimbabwe asilimia 72.3,” alisema.
Alisema kupunguza umaskini kwa nchi yoyote ile kunapaswa kuhusishwa na uwekezaji kwenye sekta nyingine za kiuchumi ambazo hugusa na kuwanufaisha wananchi walio wengi. “Nitumie fursa hii kusisitiza kuwa umaskini ni changamoto kwa dunia nzima na hasa kwa nchi zinazoendelea. Nchi zilizo na hali mbaya zaidi ni zile zilizoko Kusini mwa Jangwa la Sahara kama takwimu rasmi zinavyoonesha.”
Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu amesema ni lazima Serikali iimarishe upatikanaji wa takwimu kwa kuajiri maafisa takwimu wanaowajibika moja kwa moja na Ofisi ya Taifa ya Takwimu badala ya kumtegemea mtu anayewajibika kwa Mkurugenzi wa Halmashauri.
“Leo hii hatuna Afisa Takwimu katika kila Halmashauri, na matokeo yake hatuna mfumo mzuri wa kupata taarifa kuanzia ngazi ya chini. Tuweke utaratibu ili hawa watu wawepo na kila Afisa takwimu awajibike kupeleka taarifa yake kwa Mtakwimu Mkuu kila wakati.”
“Nilipokuwa Naibu Waziri TAMISEMI ninayeshughulikia elimu, nikiagiza takwimu fulani, kuzipata ilikuwa inachukua zaidi ya wiki mbili, na hiyo ni kwa Halmshauri moja tu. Na wakati mwingine, taarifa inakujia wakati umeshasahau kuwa ulitoa agizo uletewe.”
Mapema, akitoa taarifa juu ya utafiti huo, Mtakwimu Mkuu wa Serikali, Dkt. Albina Chuwa alisema Tanzania ni miongoni mwa nchi duniani ambazo kiwango cha umaskini kimeendelea kushuka na kufikia tarakimu moja.
Alisema utafiti huo uliofanywa na ofisi yake kwa kushirikiana na Benki ya Dunia, baadhi ya balozi na mashirika ya Umoja wa Mataifa ulilenga kupata makadirio ya viwango vya umaskini ili kufuatilia, kupima na kutathmini mipango mbalimbali ya kitaifa, kikanda na kimataifa.
Alisema katika utafiti huo, walitumia teknolojia ya kisasa iitwayo survey solution ambayo imesaidia kupunguza gharama za utafiti za kupeleka madodoso na magari. “Tulitumia vishkwambi (tablets) na kupunguza mzigo wa kubeba na makaratasi au kukaa kujumlisha taarifa,” alisema,