Waogeleaji wa timu ya Taliss-IST wakiwa katika picha ya pamoja mara baada ya kushiriki katika mashindano maalum ya kuzichangia fedha timu za Taifa za mchezo wa kuogelea ili zishiriki katika mashindano ya Dunia.
*************
Na Mwandishi wetu
Dar es Salaam. Mabingwa wa mchezo wa kuogelea nchini, Taliss- IST ya Upanga imechangia kiasi cha Sh1.5 millioni kwa ajili ya timu za taifa za mchezo huo zinazojiandaa na mashindano ya Dunia mjini Gwangju, Korea Kusini na mashindano ya vijana ya dunia yaliyopangwa kufanyika mjini Budapest, Hungary.
Klabu hiyo iliwakilisha fedha hizo katika mashindano maalum yaliyofanyika kwenye bwawa la kuogelea la shule ya sekondari ya Shaaban Robert yaliyoandaliwa na Chama cha Kuogelea Tanzania (TSA).
Taliss-IST ilichangia fedha taslimu Sh1,225,000 na dola za Kimarekani 140 katika mashindano hayo maalum ambayo yalishirikisha waogeleaji wenye umri tofauti.
Waogeleaji hao hao ni Mohameduwais Abullatif, Lara Steenkamp Aravind Raghavendran, Fallih Ahmed, Ahmed Rashid, Adam Tapya, Augustino Lucas na Hussein Ebrahim.
Wengine ni Shivani Bhatt, Sylivia Caloiaro, Nawal Shebe, Amylia Chali, Laila Rashid, Doreen Ahmed, na Zahabiya Ebrahim. Kocha wa timu hiyo, Alex Mwaipasi na Meneja, Hadija Shebe waliongoza timu hiyo katika mashindano hayo.
Waogeleaji hao waliogelea katika umbali wa kilometa 1.5 kwa mtindo wa relay, mita 400 na mita 200.
Shebe alisema kuwa wanajisikia fahari kubwa kuchangia timu ya Taifa ya wakubwa na vijana ambao wataiwakilisha nchi katika mashindano ya Dunia. TSA inahitaji jumla ya Sh 120 million kwa ajili ya kusafirisha waogeleaji wa timu ya Taifa.
Mashindano ya dunia ya kuogelea kwa wakubwa yatafanyika kuanzia Julai 12 mpaka 28 mjini Gwangju, Korea Kusini wakati mashindano uua vijana ya dunia yamepangwa kuanza Agosti 20 mjini, Budapest, Hungary.
Waogealeaji wa timu ya taifa ya wakubwa ni Hilal Hemed, Collins Saliboko ambao wanawakilisha upande wa wanaume na kwa upande wa wanawake ni Sylvia Caloiaro na Shivani Bhatt. Waogeleaji wa timu ya taifa ya vijana ni Dennis Mhini, Delvin Barick, Christopher Fitzpatrick, Christian Shirima, na Isam Sepetu ambao watashindana kwa upande wa wanaume wakati kwa upande wa wanawake ni Kayla Temba na Laila Rashid.