*************
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amesema kuanzia Julai Mosi mwaka huu Serikali itaanza kutekeleza Mpango Kazi wa Utekelezaji wa Mpango wa Kuboresha Mfumo wa Udhibiti wa Biashara nchini (Blueprint) kwa lengo la kurahisisha mazingira ya kufanya biashara.
Waziri Mkuu ameyasema hayo leo (Ijumaa, Juni 28) wakati akiahirisha mkutano wa 15 wa Bunge, jijini Dodoma. Amesema wakati kazi hiyo inaendelea Serikali itafanya ufutialiaji kuhusu utekelezaji wa mpango huo na kutathmini kama lengo limefikiwa.
”Utekelezaji wa mpango huo unakwenda sambamba na dhamira ya Serikali ya kurahisisha mazingira ya kufanya biashara nchini, unaojidhihirisha kupitia sheria ya fedha ya mwaka 2019 ambayo imefuta tozo kwamishi 54 zilizobainishwa kwenye mpango huo.”
Waziri Mkuu ametaja tozo zilizoondolewa au kupunguzwa ni pamoja na zinazosimamiwa na Shirika la Viwango Tanzania (TBS), Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA), Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali (GCLA), Wizara ya Mifugo na Uvuvi hususan kwenye Sekta ya Mifugo, Wizara ya Maliasili na Utalii na Wizara ya Maji
Kadhalika, Waziri Mkuu amesema katika kuhakikisha utekelezaji wa mpango huo unaleta tija, ameielekeza Wizara ya Viwanda na Biashara ishirikiane na Ofisi ya Waziri Mkuu kusambaza blueprint pamoja na Mpango Kazi wa Utekelezaji kwa wizara zote kwa ajili ya kusimamia utekelezaji katika maeneo yao.
Amesema kupitia mpango wa bajeti ya 2019/2020, Serikali itaendelea kuweka mazingira rahisi ya ufanyaji biashara kwa kutoa unafuu katika sekta za kilimo, mifugo, uvuvi pamoja na shughuli nyingine jumuishi.
Wakati huohuo,Waziri Mkuu amesema katika kukabiliana na kilimo tegemezi cha mvua hususani kwenye zama hizi za mabadiliko ya tabia nchi, Serikali kwa sasa inaboresha kilimo cha umwagiliaji kwa lengo la kuwatoa wananchi katika kilimo hicho.
Amesema hatua zilizochukuliwa hadi sasa ni pamoja na kuunda upya Tume ya Taifa ya Umwagiliaji ambayo inalenga kuiwezesha tume hiyo kusimamia ipasavyo shughuli za umwagiliaji. Pia Serikali imehamishia tume hiyo Wizara ya Kilimo ambayo ndiyo yenye dhamana ya kuendeleza kilimo nchini.
”Ili tuweze kufikia lengo la kuongeza eneo la kilimo cha umwagiliaji kutoka hekta 475,056 za sasa hadi hekta 1,000,000 ifikapo mwaka 2025, tayari nimeielekeza Wizara ya Kilimo isimamia kwa karibu na kutekeleza majukumu yake kwa weledi.”
Waziri Mkuu amesema Wizara ya Kilimo inatakiwa ihakikishe inasimamia vema miradi 22 ya umwagiliaji inayoendelea sasa pamoja na miradi mipya minane itakayojengwa nchini katika pindi cha mwaka wa fedha 2019/2020.