Ofisa madini Mkazi wa Mkoa wa kimadini wa Simanjiro, Daudi Ntalima (mwenye suti nyeusi) akizungumza na madalali na wafanyabiashara wa magonga ya Tanzanite Mji mdogo wa Mirerani.
Ofisa wa Tume ya madini Mirerani, Selemani Hassan akizungumzia juhudi za serikali za kuongeza wataalam na muda wa kufanya tathmini kwenye madini ya Tanzanite.
***********************
WAFANYABIASHARA wa udalali wa madini ambao leseni zao zimemaliza muda wake wametakiwa kuhuisha na kuomba upya katika shughuli itakayotumia muda wa mwezi mmoja.
Ofisa madini mkazi wa mkoa wa kimadini wa Simanjiro, Daudi Ntalima akizungumza jana mji mdogo wa Mirerani alisema zoezi hilo litaanza Julai mosi hadi Julai 25 mwaka huu.
Ntalima alisema anayedaiwa malipo ya mrabaha na ada ya ukaguzi anapaswa kukamilisha malipo yake kabla ya mwisho wa mwezi huu na hatua kali za kisheria zitachukuliwa ikiwemo kuzuiwa kuingia ndani ya ukuta.
Alisema kila mfanyabiashara wa madini ili apate leseni mpya anapaswa kuwa na jalada la taarifa getini lenye nakala ya leseni na taarifa za ununuzi na mauzo na zionyeshe mfanyabiashara mkubwa anayenunua madini hayo
“Vigezo vya kuhuisha leseni kwa wafanyabiashara wa madini ni kuwa na tin namba, kitambukisho cha mpiga kura, vielelezo vya ununuzi na uuzaji, wanunuzi wakubwa wawe na ofisi Mirerani, leseni iliyotolewa Mirerani na picha ndogo mbili,” alisema Ntalima.
Mwenyekiti wa kamati ya maadili ya wanunuzi na madalali wa madini, Victor Kunyara alisema wamelipokea agizo hilo na watalifanyia kazi kwa maslahi ya Taifa na jamii kwa ujumla.
Kunyara alisema wafanyabiashara wa madini ya Tanzanite hivi sasa wamepata elimu ya ulipaji kodi na wanalipa kodi pindi wakishauza madini yao.
Dalali wa madini Hussein Msokoto alitoa ombi kwa serikali kuhakikisha wanatoa leseni inayolingana nao ili waweze kulipa kodi na wao kujiwezesha kiuchumi na familia zao.
Msokoto alisema pia suala la wafanyabiashara kukusanyika pamoja na kutumia leseni moja linapaswa kutazamwa ili waweze kulipia na kufanya shughuli zao.
Raphael Riaga alisema changamoto ya madalali kuendelea kulipia baadhi ya kodi ikiwemo kiwango sawa cha anayelipia leseni upya na anayekata leseni upya bado inawasumbua.