Mmoja wa Mawakili akikabidhiwa Cheti cha Maudhulio na Viongozi mbalimbali wakiwemo Marais wa staafu wa chama cha Wanasheria pamoja na Mratibu Mkuu wa Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu ya Mafunzo ya siku mbili kwa Mawakili ambayo yaliandaliwa na Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania(THRDC)
Rais Mstaafu wa TLS ambaye pia ni Wakili wa Kujitegemea Bi.Fatma Karume akipokea cheti cha maudhulio ya Mafunzo kwa Mawakili hasa katika masuala ya Haki za Binadamu kuelekea Chaguzi zijazo.
***********************
NA EMMANUEL MBATILO
Mawakili ambao wamepata fursa ya kuhudhulia mafunzo kwa mawakili ambayo yameandaliwa na Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania(THRDC) wametakiwa kufanyia kazi elimu hiyo ili kuweza kutetea haki pale inapoonekana inavunjwa.
Ameyasema hayo leo Rais wa chama cha wanasheria Tanganyika (TLS),Dkt. Rugemeleza Nshala akiwa anafunga mafunzo hayo ambayo yalifanyika kwa siku mbili Jijini Dar es Salaam ambapo kulihudhuliwa na marais wa wastaafu wa chama hicho.
Dkt.Nshala amesema kuwa mafunzo hayo yatawafanya Mawakili kuelewa ni namna gani wanaweza kukabiliana na uvunjifu wa haki za binadamu hasa pale unaonevu unapotokea.
“Kitendo cha kuona haki inavunjwa nawe Wakili unaacha haki ivunjwe basi unakuwa Wakili ambaye haujui wajibu wako”. Amesema Dkt. Nshala.
Kwa upande wa Wakili wa Mahakama Kuu Zanzibar ambaye pia ni Rais Mstaafu wa Chama cha Wanasheria Zanzibar (ZLS), Bw. Awadhi Said amesema kuwa mafunzo ambayo wameyapata hasa kwa Mawakili yamekuja kwa wakati wake kwani hali iliyopo kwasasa inahitaji Mawakili wa Haki za Binadamu.
“Tujue kwamba popote pale unapoona kuna maendeleo basi kwa kiasi kikubwa Haki inatendeka na kuwa chanzo cha maendeleo hayo na pia kuna kuwepo na watu ambao wanasimama na kujitoa kutetea Haki”.
Naye Rais Mstaafu wa TLS ambaye pia ni Wakili wa Kujitegemea Bi.Fatma Karume amesema kuwa katika kuelekea chaguzi zijazo mawakili wanatakiwa kufanya kazi zao hasa katika kutetea haki pamoja na kusimamia majukumu yao vizuri paspokuangalia huyu ni nani bali wahakikishe haki inatendeka kwa wote.