Na Mwandishi wetu
Waswahili husema penye ukweli, uongo hujitenga. Usemi huu umedhihirishwa hivi
karibuni na Jarida la Kimataifa la Forbes Africa juu ya uwezo na adhima ya Tanzania katika kutekeleza miradi ya kimkakati katika kuelekea uchumi wa kati ifikapo 2025.
Uwezo mkubwa aliouonesha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli katika kuainisha miradi mikubwa ya kimkakati na kuitekeleza katika kipindi cha muda mfupi tangu aingie madarakani, imeifumbua macho dunia kuwa Rais ameamua na anaweza kuifikisha Tanzania katika uchumi wa kati ili kuwaletea maendeleo.
Akihojiwa na Jarida la Kimataifa la Forbes Africa mapema mwezi huu, Rais Magufuli alisema kuwa sio ndoto za alinacha tena, bali ni ukweli ulio wazi kuwa Tanzania imepiga hatua kubwa ya kuridhisha kuvutia wawekezaji kutoka nje kutokana na uwazi wa mifumo yake ya uwekezaji iliyo rafiki na utendaji wa kazi makini.
Jarida la Forbes limeilezea Tanzania kuwa ni sehemu salama na muuhimu kwa
wawekezaji kutoka nje huku likitaja amani, mazingira mazuri ya uwekezaji, uongozi madhubuti unaosimamia misingi ya kuboresha hali ya uwekezaji, biashara na miundombinu rafiki kwa uwekezaji kama nyenzo muhimu katika ukuaji wa uchumi.
“Ukuaji wa sekta ya usafirishaji na kuweka mifumo bora ya usimamizi imeifanya
sekta hii kukua kutoka asilimia 4.4 mwaka 2012 hadi kufikia asilimia 16.6 mwaka 2017 ambayo imeongeza pato la Taifa hadi kufikia asilimia 6 mwaka 2017”, amesema Rais Magufuli.
Katika Jarida hilo, Rais Magufuli ametaja miradi inayojenga mazingira ya kuboresha uwekezaji kuwa ni pamoja na mradi wa ujenzi wa miundombinu na upanuzi wa Bandari, viwanja vya ndege na barabara inayounganisha mikoa, wilaya na vijiji, uwepo wa nishati ya umeme mpaka vijijini, mfano wa Mtambo wa kusafirisha umeme wa njia kuu ya Makambako – Njombe na mradi mkubwa wa umeme wa mto Rufiji unahakikishia wawekezaji umeme wa uhakika.
Ukuaji huu sio kwamba unaonekana na watanzania tu bali nchi zote za Kanda ya
Maziwa Makuu ambazo hazina bandari na zinategemea sekta ya usafirishaji ya
Tanzania kuwahudumia wamepongeza mara zote kwa uboreshaji na urahisishaji wa usafiri katika kipindi cha miaka minne ya uongozi wa Rais Magufuli.
Nchi wanachama wa ukanda huo wamempongeza Rais Magufuli kutokana na jitihada hizo na namna Bandari ya Dar-es-salaam inavyohudumia na kusafirishwa kwa haraka bila ya vikwazo, kupungua kwa vituo vya ukaguzi na gharama nafuu za usafirishaji zinazopunguza gharama za bidhaa huku kiwango cha biashara kikikua zaidi.
Kwa sasa bandari ya Dar-es-Salaam imeongeza uwezo wa kushusha na kupakia mizigo kwa mwaka tani 28 elfu na inafanya kazi saa 24. Vilevile, uthubutu na utayari wa Rais Magufuli kukutana na wawekezaji, wafanyabiashara na kusikiliza changamoto za uwekezaji na kuzitatua mara moja billa urasimu na rushwa ni kivutio kikubwa kwa wawekezaji kuwekeza Tanzania.
Akiongezea Rais Magufuli ameleezea eneo lingine ambalo ni muhimu kwa uwekezaji na kuboresha hali za maisha ya watanzania kwa ujumla la kuongezwa umeme wa uhakika katika mradi wa Kinyerezi II (240 MW) wa gesi asilia, mradi mkubwa wa umeme wa mto Rufiji wa Mega Watt 2115 na Mtambo wa usafirishaji umeme wa Kilo Volt 400 (Backbone Transmission Investment Project – BTIP); na Mtambo wa Usafirishaji wa Kilo Volt – 220 kutoka Makambako – Songea; na miradi mengine ya umeme vijijini 6,349.
Ambapo, miradi yote hiyo inafanya kuwa na uhakika wa kuwa na umeme wa uhakika ambao unaleta maendeleo ya kiuchumi na kijamii katika Taifa letu. Amesema Rais Magufuli.
Akimalizia mahojiano yake Rais Magufuli amesema kuwa anaona fahari kwa kuboresha maeneo ya makubwa ya huduma za jamii kama afya, elimu, umeme na maji. Pia, tumeondoa urasimu katika utendaji wa serikali kuweka maadili ya kiutumishi, na kuondoa rushwa katika maeneo yote na uchumi wetu umekuwa kwa asilimia saba.
Tunaendelea kuboresha mazingira ya uwekezaji kwa sekta zote, biashara na
kuboresha mifumo ya utendaji kazi kidigitali.
Naye Waziri wa Maliasili na utalii Dkt, Hamisi Kingwangwala ametumia fursa hiyo ya kuhojiwa na Jarida la Forbes kutangaza fursa ya kuwekeza katika ujenzi wa miji mitatu ya kitalii, ambapo mmoja utakuwa Hifadhi ya Saadani na nyingine mbili
zitakazojengwa karibu na Hifadhi za Taifa.
Dkt Kigwangala amesema “Kutokana na mtandao mzuri wa barabara, viwanja vya
ndege na train, mitandao rahisi ya haraka ya mawasiliano na vivutio vizuri vya
kipekee duniani kuna kila sababu ya wawekezaji kuja kuwekeza Tanzania”.
Akiongelea sekta ya fedha Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania-BOT, Profesa Florens Luoga amesema kuwa, ili kuvutia uwekezaji na kuboresha sekta ya fedha uwekaji wa mfumo wa kimtandao na ukuwaji wa sekta ya fedha Tanzania ni kivutio muhimu kwa wawekezaji kutoka nje kuwekeza nchini.
Prof. Luoga amesema: “Dhima na muelekeo wa BOT ni kuhakikisha mfumo wa fedha nchini unakuwa wenye manufaa kwa kukuza mitaji ya sekta binafsi na kupunguza vihatarishi katika mikopo”.
Aidha, ongezeko wa mikopo kwa wafanyabiashara na wawekezaji imekuwa kutoka asilimia 0.8 kutoka mwaka 2017 mapaka 4.8 mpaka septemba 2018. Ambapo kuna ongezeko kidogo, lakini sio matarajio ya BOT, hivyo ili iongezeke zaidi tunafanya jitihada za kurekebisha mifumo ili iwe rafiki zaidi kwa mabenki waweze kuwa na taarifa sahihi za wateja wao kuepuka viatarishi visivyo vya lazima. Amesema Prof Luoga.
Akijibu swali kwa nini wakati huu ni muhimu sana wawekezaji kuja kuwekeza
Tanzania Prof. Luoga amesema zipo sababu nyingi lakini uongozi makini na wenye
kujitambua unataka nini (commitment) ameongeza prof Luoga,
Yote yanayoonekana katika utekelezaji wa uwekezaji na bishara kwa sasa ni matokeo ya juhudi ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt Magufuli kuweka mazingira mazuri na kuwasikiliza mara kwa mara wawekezaji na wafanyabiashara.Amemalizia Prof Luoga.
Akiongea na Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya Shelys Pharmaceuticals Company Dkt
Sanjay Advani amesema, “Kwa sasa ni wakati muafaka kuwekeza katika sekta ya
utengenezaji wa dawa za binadamu, vitendanishi na vifaa vya huduma ya Afya kwa sababu serikali yenyewe ndio imehamasisha utengenezaji huo na kuondoa kodi zilizokuwa kikwazo na soko lipo kubwa kabisa na wazi”.
Miradi mikubwa ya kimkakati inahakikishia wawekezaji Tanzania ijayo ndani ya muda mfupi hakuna kitakachoshindikana, uwepo wa ujenzi wa reli ya kisasa ya umeme Dar- es-salaam- mpaka Morogoro, sambamba na kuendelea kwa reli ya zamani katika usafiri inawahakikishia wawekezaji popote utakapowekeza miundombinu ya uasafiri ni rafiki.
Hili ni funzo la kujifunza kwa wale wanaobeza kila kinachofanywa na serikali hususan katika miradi mikubwa ya kimkakati kuwa ni chanzo cha mzunguko mdogo wa fedha na kuwafanya watanzania wakose fedha mifukoni la hasha!!!. Ninadhani ndio wale aliowasema Mheshimiwa David Kafulila kuwa walizoea uchumi wa ‘misson town’ badala ya kwenda kwa uchumi halisi.
Uchumi halisi ndio aliouelezea Rais Magufuli katika mahojiano yake na Forbes Africa, adhima, lengo na madhumuni yake binafsi kama kiongozi na maelekezo ya ilani ya chama chake katika kuitekeleza miradi mikubwa ya kimkakati. Miradi iliyofanyiwa utafiti wa kina kuwa ndio mwanzo wa kuipeleka Tanzania katika uchumi wa kati ifikapo 2025.
Watanzania tubadilike, mtu anapokueleza jambo hebu dadisi, uliza kwa watu
mbalimbali wenye weledi wa jambo husika ili kupanua uwezo wako wa kupambanua masuala mbalimbali ambayo kimsingi hata wewe binafsi kama mtanzania yana manufaa kwako.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akishirikiana na Balozi wa Jamhuri ya Korea nchini Mhe. Cho Tae-ick kufunua pazia kuashiria kuwekwa kwa jiwe la Msingi la Mradi wa Ujenzi wa Daraja Jipya la Selander na Barabara unganishi ya Km 6.23 toka Hospitali ya Aga Khan hadi ufukwe wa Coco Beach jijini Dar es salaam leo Desemba 20, 2018. Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa, Mama Janeth Magufuli na viongozi wengine wanashuhudia.