Mwenyekiti wa Kamati ya uongozi ya (MKURABITA ) Balozi mstaafu Daniel Ole Njolay akimkabidhi Bw. Said Yahya Mkaazi wa Mpendae Hati yake ya Ardhi katika hafla iliyofanyika huko Mpendae mjini Zanzibar. Kulia ni Mrajisi wa Ardhi Zanzibar Dk. Abdul-Nasser Hikmany
Mzee Omar wa Mpendae kushoto akionesha Hati yake ya Ardhi aliyokabidhiwa na Mwenyekiti wa Kamati ya uongozi ya (MKURABITA ) Balozi mstaafu Daniel Ole Njolay (katikati Mwenye Kaunda Suti) hafla ya kukabidhi hati hizo ilifanyika Mpendae mjini Zanzibar. Kulia ni Mrajisi wa Ardhi Zanzibar Dk. Abdul-Nasser Hikmany
Mkuu Wizara ya Ardhi Maji Nishati na Mazingira Ali Khalil Mirza akizungumza na Wajumbe wa Kamati ya Uongozi ya MKURABITA walipomtembelea Katibu huyo Ofisi kwake Forodhani mjini Zanzibar . Picha na Faki Mjaka-Maelezo Zanzibar
****************
Na Faki Mjaka-Maelezo Zanzibar 26.06.2019
Mwenyekiti wa Kamati ya uongozi ya Ofisi ya Mpango wa kurasimisha Rasilimali na Biashara za Wanyonge (MKURABITA ) Balozi mstaafu Daniel Ole Njolay amewataka Wananchi waliokabidhiwa Hati za Ardhi kuzitumia vyema kwa ajili ya kuombea Mikopo itakayowasaidia kupambana na umasikini wa kipato.
Balozi Njolay ametoa wito huo katika hafla ya kuwakabidhi Wananchi 54 wa Mpendae mjini Zanzibar Hati hizo mara baada ya kukamilisha masharti ya usajili.
Amesema Serikali ya Muungano kwa kushirikiana na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar zimeazimia kuwakomboa Wananchi wake na umasikini wa kipato kupitia njia mbali mbali ikiwemo kuwapatia Hati za Ardhi zitakazowasaidia katika harakati zao za kimaendeleo.
Amewataka Wananchi hao kuzitumia Hati hizo ili kuomba Mikopo kutoka vyanzo mbalimbali vya kifedha ikiwemo Benki kwa ajili ya kuendeshea maisha yao.
“Wenzetu nje ya nchi Hati hizi zinakuwepo katika Bank huzitumia kikamilifu kukomba Mikopo ya kuwasaidia kuendeleza miradi yao ya kimaendeleo ambayo wanaianzisha hivyo hapa Tanzania tunawajibu wa kuyaiga hayo ” amefahamisha Balozi Njolay.
Kwa upande wake Mratibu wa MKURABITA Tanzania Dkt. Seraphia Mgembe amewaomba Wananchi hao hasa Wazee kuzitumia Hati hizo ili kukamilisha ndoto zao walizoshindwa kuzifanya wakati wa ujana wao.
Amesema kabla ya kupata Hati hizo kuna mambo mengine muhimu walishindwa kuyatekeleza kwa kukosa Mikopo hivyo kupitia hati hizo wana uwezo wa kuzitumia kukamilisha ndoto zao.
Amesema ili Mwananchi awe na uchumi mzuri kunahitajika mipango endelevu itakayomsaidia kupata Mtaji wa kufikia maendeleo aliyoyajipangia.
“Inawezekana mmoja wenu alitamani kufanya mambo makubwa lakini akashindwa kwa kukosa kielelezo cha Hati ambacho kingemfanya kupata Mkopo hivyo kuanzia leo hata kama ni Mzee fursa sasa unayo ya kukopa ukafanya mambo yako unayoamini bado ni muhimu” Alishauri Dkt. Seraphia
Kwa upande wake Mrajisi wa Ardhi Zanzibar Dk. Abdul-Nasser Hikmany amewataka Wananchi waliopatiwa hati hizo kuzitumia vyema ili zilete mabadiliko ya kiuchumi kwa kuzitumia katika kutafuta Mitaji kutoka taasisi za kifedha nchini.
Amesema mwelekeo wao ni kuhakikisha maeneo yote Unguja na Pemba yanapimwa na Wamiliki wake kupatiwa Hati ambazo watazitumia kama rasilimali muhimu na kupunguza migogoro ya Ardhi.
Mmoja wa waliokabidhiwa Hati hiyo Mmanga Omar ameishukuru Serikali kwa kutoa Hati hizo ambazo zitakuwa kielelezo muhimu cha wao kupata misaada mbali mbali ya kujiendeleza na maisha.
Amesema ataitumia kama fursa muhimu ya kukopa Bank ili kuwatengenezea mustakabali mwema watoto wake ikiwemo kuwasomesha na kuwafungulia biashara.
“Pamoja na kwamba kukopa si kipaumbele sana lakini katika utaratibu uliowekwa sasa zipo Bank za Kiislam nazo zinakopesha hivyo tutazitumia ili kutengeneza future ya Watoto wetu” alisema
ameishauri Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kuharakisha utoaji wa Hati hizo kwa Wananchi wengine Unguja na Pemba ili kuchangamkia fursa zinazoweza kupatikana kupitia umiliki wa Hati hizo.
kupunguza gharama za uanzishwaji wa biashara kwa wananchi ikiwemo ukataji wa Leseni ili kuyafanya mazingira ya biashara kuwa rahisi.
Awali Wajumbe wa Kamati ya Uongozi ya MKURABITA walimtembelea Katibu Mkuu Wizara ya Ardhi Maji Nishati na Mazingira Ali Khalil Mirza na kumuelezea changamoto walizokutana nazo zinazodumaza maendeleo ya Wananchi wa Zanzibar.
Kamati hiyo ipo Zanzibar ikiendeleza ziara yake ya siku tano kukagua shughuli mbali mbali zinazofanywa na MKURABITA visiwani Zanzibar kwa lengo la kusaidia kutatulia changamoto zinazowakabili Wananchi hasa katika Nyanja za kibiashara na ardhi.