Washiriki wa Kambi ya Ariel 2019 wakicheza katika ukumbi wa Landmark Hotel Jijini Dar es salaam Juni 24,2019
Mwezeshaji Kiongozi, Mgunga Mwamnyenyelwa akitoa mada kwenye kambi ya Ariel inayofanyika jijini Dar es salaam
**
Baadhi ya wazazi wamekuwa wakiwapa watoto wao wanaoishi na VVU dawa za kupunguza makali ya VVU bila kuwaeleza kuwa dawa hizo zinatibu nini hali inayochangia watoto hao kuacha dawa hizo kutokana na kutokujua umuhimu wake.
Hayo yameelezwa na watoto na vijana kutoka mikoa ya Mara, Shinyanga, Simiyu na Mwanza wanaoshiriki Ariel Camp 2019 iliyoandaliwa na asasi inayolenga kutokomeza UKIMWI kwa watoto na familia, Ariel Glaser Pediatric AIDS Healthcare Initiative (AGPAHI).
Wakizungumza kwenye kambi hiyo inayofanyika katika hoteli ya Landmark, jijini Dar es Salaam, watoto walisema kutokuwaambia watoto ukweli kuhusu kuishi kwao na VVU ni moja ya sababu zinazofanya watoto hao waache kutumia dawa hizo muhimu.
“Utakuta mzazi anampa mtoto dawa za ARV kila siku lakini hamwelezi kuwa hizo dawa ni za ugonjwa gani. Watoto wakiuliza dawa hizo ni kwa ajili ya nini wanaambiwa ni za kifua ama za kuongeza akili,” alisema mtoto mmoja kutoka Simiyu na kuungwa mkono na wenzake.
“Kutomwambia mtoto ukweli si sahihi kwani kunamfanya asijue umuhimu wa dawa hizo kwa maisha yake. Pia mtoto asipoambiwa ukweli kuhusu hali yake ni hatari kwani pindi atakapojua ukweli anaweza kuchukua maamuzi mabaya hivyo tunaomba wazazi wasiwafiche watoto wao,” aliongeza mtoto wa Mwanza.
Watoto hao walitoa wito kwa wazazi na walezi ambao wanaendekeza waganga wa kienyeji badala ya kumpeleka mtu hospitali anapoumwa. Walisema kuwa kutokana na kuwapeleka kwa waganga hao wagonjwa, wazazi na walezi wamekuwa wakidanganywa kuwa mgonjwa amerogwa.
Walisema matokeo ya kupelekwa mgonjwa kwa mganga wa kienyeji ni kukosa huduma sahihi za afya hali inayosababisha kupoteza maisha hivyo kuchangia vifo vingi vya watu wanaoshi na maambukizi.
Na Kadama Malunde – Malunde1 blog