Tayari Bandari ya Lushamba imeshaanza kuwanufaisha wavuvi na wasafiri.
……………………………………………………..
Basi tulirejea jijini Mwanza kuendelea na uchakataji wa habari ili ziwe tayari kwa kutumika kwenye vyombo vyetu siku hii ikawa imeisha.
Ratiba ya siku iliyokuwa inafuata Juni 5 ilikuwa ni safari ya kwenda Sengerema ambako wananchi wa Lushamba hawakuwa na bandari tangu mwaka 1958 sasa wamejengewa baada ya miaka 61 kupita, Je? wananchi wanasemaje kuhusu Rais Dkt. John Pombe Magufuli.
Wananchi mabimbali wa Lushamba walimshukuru sana Rais Dkt John Magufuli kwa kuwajengewa bandari hiyo kwani wamekuwa katika adha ya kukosa usafiri kwa miaka mingi, hivyo kukamilika kwa bandari hiyo ni ukombozi kwao katika Usafiri, Uvuvi, Biashara masuala ya afya ambapo pia wanatarajia kupata fursa zitakazo wafungua kiuchumi kwa ujumla wake.
“Tunashukuru serikali kwa kutukumbuka kwa ujenzi wa bandari ya Lushamba ambayo itarahisisha usafiri wa kwenda na kutoka katika kijiji hicho ambacho kwa miaka mingi kumekuwa na changamoto nyingi,”
Maneno haya yanatoka kinywani mwa Mwenyekiti wa Serikali ya Kijiji hicho, Lazaro Mgonzo wakati Akizungumza na waandishi wa habari katika bandari hiyo iliyopo katika Kijiji cha Kanyala, anasema kuanzia mwaka 1958 hakukuwa na usafiri wa kwenda kisiwani hivyo kuanza kwa usafiri huo utatatua changamoto hiyo.
Kukamilika kwa mradi wa ujenzi wa gati la Bandari ya Lushamba uliogharimu Sh. bilioni 1.265 ambazo ni fedha za ndani ni faraja kubwa kwa wakazi hao,Bandari hiyo itaanza kutumika Julai mwaka huu baada ya usafiri huo kuwa wa kusuasua tangu mwaka 1958.
Baada ya kutoka katika Bandari ya Lushamba kijiji cha Kanyala tuliondoka katika jimbo la Buchosa wilaya ya Sengerema mkoani Mwanza na kuelekea mkoani Geita ambako tulitembelea bandari kongwe ya Nyamirembe, Wilaya ya Chato mkoa wa Geita ambayo ilijengwa wakati wa iliyokuwa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) kabla ya kuvunjika.
Ujenzi wa bandari ya Nyamirembe unaelelea
……………………………………………..
Watu wengi wanadhani bandari hiyo ndiyo inajengwa sasa na Serikali ya awamu ya tano La hasha, Bandari ya Nyamirembe ilikuwepo muda mrefu na iliendelea kufanya kazi kwa muda mrefu.
Injinia wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari (TPA), Kanda ya Ziwa Victoria, Abraham Msina “Katika gati hili, meli ziliacha kuja miaka minane sababu kampuni iliyokuwa inaleta meli hizo ilisitisha kwa sababu zao wenyewe lakini Kampuni ya Huduma za Meli (MSCL) wameurudisha tena mradi huu,” alisema
Akizungumza na waandishi wa habari bandarini hapo , Injinia Abraham Msina aliongeza kuwa mradi huo unaendelea na uko katika hatua ya asilimia 40 ya utekelezaji.
Alisema sehemu ya kazi iliyobakia ni kumalizia ujenzi wa gati, jengo la abiria, jengo la mizigo, chumba cha mashine ya umeme, vyoo na chumba cha walinzi.
Msina alisema bandari hiyo itakapoanza kazi itachochea biashara kati ya nchi za Rwanda, Burundi, Uganda na Kenya.
Ujenzi wa mradi huo unagharimu Sh. bilioni 4.1 ambazo ni fedha za serikali, unajengwa na Mkandarasi wa ndani ambaye ni Kampuni ya VJ Mistry, kutoka Bukoba mkoani Kagera ambapo unatarajiwa , kukamilika Agosti 23, mwaka huu.
Naye mwakilishi wa Mkandarasi wa mradi huo, Injinia Anderson Mbogowe alisema mradi huo umefikia asilimia 47 na wanatarajia kukamilisha kazi hiyo Julai na kisha kukabidhi kwa serikali Agosti mwaka huu.
Tulipomaliza kutembelea Bandari za Lushamba wilayani Sengerema mkoani Mwanza na Nyamirembe wilaya ya Chato Mkoani Geita ratiba ilikuwa inatupeleka moja kwa moja mkoani Kagera ambako tungelala na kuanza kazi huko kesho yake.
Katika safari ile tuliyoanza safiri jua likiwa limezama na giza limeshaingia kulikuwa na utani mwingi moja ya mambo yaliyokuwa yakijadiliwa ni kupita eneo la pori la Kasindaga ambalo ni hatari wakati mwingine kutokana na uhalifu unaowatokea wasafiri nyakati za usiku.
Vijana wangu akina Willy , Hillay, Kamugisha na wengine wakawa wanajadiliana hivi tukivamiwa kiongozi wetu inabidi awe nani? Wengine wakasema inabidi awe mtu mzima kwenye hili gari, Wengine wakasema tutawaambia kwamba mtu mzima humu ndiyo kiongozi wetu eti niwe mimi kwa sababu nina mvi zangu za ukoo.
Wengine wakasema Kiongozi atakuwa Shayo kwa sababu yeye kakaa mbele na dereva Hassan Shaban basi utani ukawa hivyo, huku tukicheka na kufurahia safari
Ghafla likatokea balaa moja, Ng”ombe kaingia Barabarani Duuh!! huku na kule Dereva Hassan Shaban akajitahidi kukwepa lakini wapi Kioo cha kushoto (Side Mirror) kikamparuza yule Ng’ombe gari likayumba sana, lakini Dereva alikuwa makini akadhibiti usukani gari likakaa sawa, Mungu saidia tukaendelea na safari yetu.
Katika sekeseke hilo tayari vijana walichanganyikiwa ndani ya gari wakadhani kimeshawaka wakakaa kimyaa, tukatembea kama mita 200 hivi ndiyo zikaanza kusikika sauti vicheko kidogo na mazungumzo, Hata hivyo kwa uwezo wa mwenyezi Mungu tuliingia mjini Bukoba tukiwa salama salimini……………………….INAENDELEA
ENDELEA KUFUATILIA SIMULIZI HII NITAKUSIMULIA MAAJABU YA RAIS MAGUFULI NILIYOYAONA.