Mhandisi Suk-Joo Lee kutoka katika kampuni ya Yooshin Engineering akimueleza Rais Magufuri namna ujenzi wa daraja la Tanzanite ukiendelea kufanyika
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Magufuri akiwa katika eneo ambalo ujenzi wa daraja la Tanzanite ukiendelea baada ya kufanya ziara ya kushtukiza katika ujenzi huo.
***********************
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli leo tarehe 24 Juni, 2019 amefanya ziara ya kushtukiza katika mradi wa ujenzi wa daraja linalokatiza baharini kwa kuunganisha maeneo ya Aga Khan na Coco Beach Jijini Dar es Salaam kwa lengo la kujionea maendeleo ya ujenzi wa daraja hilo.
Mhe. Rais Magufuli ameshuhudia shughuli za ujenzi zikiendelea vizuri ambapo mkandarasi ambaye ni kampuni ya GS Engineering ya Korea anakamilisha kuunganisha daraja la muda litakalomwezesha kuanza ujenzi wa nguzo za daraja. Kwa ujumla kazi imefikia asilimia 10.12.
Akiwa katika mradi huo Mhe. Rais Magufuli amekutana na Mhandisi Mshauri kutoka kampuni ya Yooshin Engineering Mhandisi Suk-Joo Lee na kumuelezea kufurahishwa kwake na maendeleo ya ujenzi wa daraja hilo ambalo linatarajiwa kusaidia kupunguza msongamano wa magari kutoka na kuingia katikati ya Jiji la Dar es Salaam.
Nae Bw. Suk-Joo Lee ameelezea kufurahishwa kwake kufanya kazi Tanzania na ameahidi kuwa kazi hiyo itakwenda vizuri.
Daraja hilo litakuwa na urefu wa kilometa 1.03 na barabara za kuunganisha zenye urefu wa kilometa 6.23. Ujenzi wake unahusisha ujenzi wa nguzo za msingi zenye urefu wa kati ya meta 14 na 65 na utagharimu takribani shilingi Bilioni 255.
Daraja hilo limependekezwa kuitwa Tanzanite Bridge na litakamilika Oktoba 2021.