Wachezaji Hamis Ismail (mgongoni 12) na Bakari Morris saimon (13) wa Mtwara wakitafuta mbinu za kuwazuia washambuliaji hatari wa timu ya soka ya mkoa wa Lindi wakati wa pambano la fungua dimba lililochezwa jana Uwanja wa Nangwanda Mtwara. Lindi ilishinda 2-0.
Baadhi ya wanariadha wa mikoa mbalimbali ambao walishiriki mbio za mchujo mita 1500 wakipambana vikali leo asubuhi katika viwanja vya chuo cha ualimu Mtwara
Baadhi ya washiriki wa mashindano ya UMITASHUMTA kutoka mkoa wa Songwe wakipita mbele ya mgeni rasmi jana kwenye uwanja wa Nangwanda mjini Mtwara
**********************
Na Mathew Kwembe, Mtwara
Timu za soka za wasichana kutoka mikoa ya Kilimanjaro na Manyara zimeaanza kwa kishindo kwenye mashindano ya Umoja wa Michezo na Taaluma kwa Shule za Msingi Tanzania UMITASHUMTA ambayo yameanza katika viwanja vya chuo cha ualimu Mtwara.
Katika michezo iliyochezwa leo asubuhi, Kilimanjaro iliichapa bila huruma timu ya mkoa wa Ruvuma kwa magoli 4-0, huku Manyara nayo ikitoa kipigo kama hicho kwa majirani zao wa Arusha.
Matokeo mengine yanaonyesha Mwanza ikiichabanga Iringa 3-0, Tabora ikiifunga Simiyu kwa goli 1-0, Mara ikipata ushindi wa chee baada ya timu ya soka wasichana ya singida kutotokea uwanjani huku Geita akitoka sare na Kagera kwa magoli 2-2, Dare es salaam na Lindi zikitoka sare ya magoli 1-1.
Kwa upande wa mpira wa miguu (soka maalum) Kigoma ilifungwa na Njombe kwa magoli 1-3, Shinyanga nayo ilichapwa na Kilimanjaro kwa magoli 2-3, Manyara imeichabanga bila huruma Katavi magoli 7-0, Mwanza ilifungwa na Dodoma kwa magoli 0-1 huku Tanga ikiifunga Geita magoli 4-1, Iringa ikiichapa Mara 1-0 na Dar es salaam ikifungwa ba Ruvuma 0-1.
Katika mchezo wa kurusha tufe kwa upande wa wasichana mshindi wa kwanza ambaye atajinyakulia medali ya dhahabu ni Fadhila Ponela wa Lindi, medali ya fedha imechukuliwa na Katherine Amri wa Tabora na medali ya shaba imekwenda kwa Mariam Kisenge wa Simiyu.
Matokeo ya mchezo wa tufe wavulana yanaonyesha kuwa mshiriki Alex Selestine wa Dodoma amejinyakulia medali ya dhahabu, George Domel wa Manyara akipata medali ya fedha huku medali ya shaba ikichukuliwa na mshiriki Moses Alfred kutoka mkoa wa Dodoma.