Home Mchanganyiko WAZIRI LUGOLA ASHANGAA MAHABUSU 11 WALIOFUTIWA KESI MAHAKAMANI KUWEPO KITUO CHA POLISI...

WAZIRI LUGOLA ASHANGAA MAHABUSU 11 WALIOFUTIWA KESI MAHAKAMANI KUWEPO KITUO CHA POLISI KWA MIEZI SITA

0

 

Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Kangi Lugola (kushoto) akimuhoji mwananchi aliyekuja kumchukulia dhamana ndugu yake katika Kituo cha Polisi Gogoni, jijini Dar es Salaam, leo. Lugola alifanya ziara ya kushtukiza kituoni hapo kwa ajili ya kukagua utendaji kazi.

Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Kangi Lugola (kulia) akikagua Bodaboda mbalimbali katika Kituo cha Polisi Gogoni, Wilaya ya Kipolisi Kimara, jijini Dar es Salaam. Lugola alifanya ziara ya kushtukiza kituoni hapo, leo kwa ajili ya kukagua utendaji kazi.

Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Kangi Lugola akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kumaliza ziara yake ya kushtukiza aliyoifanya Kituo cha Polisi, Wilaya ya Kipolisi Kimara, jijini Dar es Salaam. Lugola alifanya ziara ya kushtukiza kituoni hapo, leo kwa ajili ya kukagua utendaji kazi.

Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Kangi Lugola akizungumza na viongozi wa Wilaya ya Kipolisi Kimara, jijini Dar es Salaam, leo, wakati alipofanya ziara ya kushtukiza Kituo cha Polisi Gogoni, jijini Dar es Salaam kwa ajili ya kukagua utendaji kazi kituoni hapo. Picha na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi.

………………..

Na Mwandishi Wetu, MOHA

WAZIRI wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Kangi Lugola amepatwa na mshangao baada ya kuwakuta mahabusu 11 wa mauaji ambao walifutiwa kesi na mahakama, kuwepo Kituo cha Polisi Gogoni, kwa muda wa miezi sita.

Lugola alifanya ziara ya kushtukiza katika Kituo hicho kilichopo Wilaya ya Kipolisi Kimara, Wilayani Ubungo, jijini Dar es Salaam, leo kwa lengo la kuangalia utendaji wa Polisi kituoni hapo, mara baada ya kuwahoji mahabusu 32 kituoni hapo akakutana na mahabusu hao ambao baadhi yao walifungwa miaka saba Gerezani.

“Kituo hiki cha Gogoni kwa mujibu wa taarifa nilizo nazo kinaongoza nchini kwa kukaa na mahabusu kwa muda mrefu, sasa hili la mahabusu 11 waliofutiwa kesi kuwepo kituoni hapa hii si sawa, na pia linanishangaza,” alisema Lugola.

Amesema viongozi wa Polisi Wilaya wamempa taarifa ya uwepo wa mahabusu hao, amewapa maelekezo kulifanyia kazi tukio hilo, naye ameahidi kuichukua changamoto hiyo na uongozi wa  Wizara kuifanyia kazi haraka iwezekanavyo.

“Kuna malalamiko ya vituo kukaa na watuhumiwa bila kupelekwa mahakama na kituo hiki  kinaongoza kwa kukaa na mahabusu kwa muda mrefu na leo Juni 23, 2019 nimekuta mahabusu 32, wakiwemo mahabusu hawa 11 ambao wameniletea mshangao,” alisema Lugola.

Lugola aliongeza kuwa, lengo la ziara zake ni kukagua na kuona ufanisi wa namna Jeshi la polisi linavyotoa huduma kwa wananchi na kuwasikiliza maoni ya wananchi juu ya huduma wanazozipokea kutoka kwa jeshi hilo.

Waziri Lugola amesema serikali ya awamu ya tano chini ya uongozi wa Rais Dkt. John Magufuli kupitia ilani ya Chama Cha Mapinduzi iliyodhamiria kupambana na umaskini na changamoto ya ajira, Serikali ipo makini na wanahakikisha wananchi wanapambana na umaskini na tatizo la ajira.

Aidha, amesema vijana wengi wameamua kupambana na umaskini kwa kujiajili kupitia pikipiki maarufu bodaboda lakini kumekuwa na malalamiko mengi ambayo yalifika hadi bungeni kwa vijana hao kuonewa, kupigwa na kunyang’anywa pikipiki zao.

“Nilitoa maagizo kwa Jeshi la Polisi juu ya bodaboda ambazo zinaweza kukamatwa na kuwekwa katika vituo vya polisi; bodaboda  zinazostahili kukamatwa ni zile zilizohusika na uharifu, zilizohusika na ajali, zilizopotea na kuonekana na zile zilizookotwa,” alisema Lugola.

Aliongeza kuwa, bodaboda nyingine zinazokamatwa na makosa mengine ya usalama barabarani kwa kupakia abiria zaidi ya mmoja maarufu kama mshikaki na kutovaa kofia ngumu na mshtakiwa anaweza kutozwa faini ambayo italipwa ndani ya siku saba.

Hata hivyo, Waziri Lugola baada ya ziara yake hiyo ambapo alizikagua bodaboda m,balimbali kituoni hapo, alisema amejiridhisha kwa kukuta bodaboda zote zipo kwenye makundi aliyoyaainisha na amelipongeza na amempongeza Mkuu wa Jeshi hilo, Simon Sirro kwa maelekezo yake aliyoyatoa kwa Jeshi hilo kufanyiwa kazi.