Meneja wa Wakala wa Vipimo Shinyanga Bw. Elias Nyanda akihakiki mizani inayotumika katika ununuzi wa pamba kwenye chama cha msingi cha ushirika (AMCOS)
Afisa Vipimo Shinyanga akitoa elimu ya matumizi sahihi ya mizani kwa Wakulima wa Pamba
Meneja wa Survaillance Bw. Moses Ntungi akiwaelekeza wakulima wa Pamba namna ya kuhakiki seal zilizofungwa katika mizani kabla ya kupima pamba zao.
Meneja wa Wakala wa Vipimo Shinyanga Bw. Elias Nyanda akitoa elimu kwa Wakulima wa Pamba
Meneja wa Wakala wa Vipimo Shinyanga Bw. Elias Nyanda akitoa elimu kwa Wakulima wa Pamba
………………………..
Wakala wa Vipimo (WMA) Mkoa wa Shinyanga inaendelea na zoezi la utoaji elimu kwa Wakulima wa pamba katika wilaya ya Kahama kwa lengo la kuwawezesha wakulima wawe na elimu ya utambuzi wa mizani sahihi zilizo hakikiwa na Wakala wa vipimo na kuwekewa stika pamoja na lakiri (seal) inayofungwa katika njia za kuingilia kwenye mizani ili kuzuia isichezewe na wafanyabiashara wasiyo waaminifu kwa lengo la kujiongezea faida zaidi.
Wakala wa Vipimo Mkoa wa Shinyanga kabla ya kuanza kwa msimu wa ununuzi wa pamba ilifanya uhakiki wa mizani zote zitakazotumika katika vyama vya msingi vya ushirika (AMCOS) 195 zilizopo katika Halmashauri za Ushetu, Kahama Mji, Msalala, Kishapu, Shinyanga DC pamoja na Manispaa ili kuhakikisha Wakulima wanauza pamba kwa kutumia vipimo vilivyo sahihi.
Akizungumza na mwandishi wetu Meneja wa WMA Shinyanga Bw. Elias Nyanda amesema, mpaka sasa jumla ya kata 20 katika wilaya kahama zimepatiwa elimu ya matumizi sahihi ya vipimo na ukaguzi wa mizani umeendelea kufanyika katika vituo vinavyotumiwa kuuzia pamba ili kujiridhishsa kama mizani hizo zinafanya kazi kwa usahihi ili kumsaidia mkulima aweze kupata fedha kulingana na thamani ya pamba anayouza.
Bw. Nyanda amesema katika zoezi hilo la elimu wakulima wameelimishwa wawe makini pindi wanapoenda kuuza pamba kwa kuhakikisha mizani inasoma sufuri (0) kabla ya kuanza upimaji kwa kutumia mizani ya digitali. Mara baada ya kupima furushi la pamba mizani inatakiwa kurudi katika sufuri, na wahakikishe mizani haisomi hasi (-) baada ya kutoa mzigo na ikitokea imesoma hasi mwambie karani anayesimamia mizani aweze kuizima na kuiwasha tena mizani hiyo kisha zoezi la upimaji liendelee.
Akizungumza na mwandishi wetu Mkulima wa pamba Bw. Joseph Nyamwanga ameipongeza sana Wakala wa Vipimo kwa elimu wanayowapatia kwani imewasaidia sana hasa katika kupunguza pointi zinazojitokeza wakati wa upimaji na kubakisha namba kamili. Amesema wataendelea kuwa makini na kuitumia elimu hiyo ili waweze kupata haki wanayostahili kila wanapoenda kuuza pamba katika AMCOS.
Meneja Nyanda pia ameeleza kuwa kwa sasa sheria ya Vipimo Sura Na. 340 na mapitio yake ya mwaka 2002 imeboreshwa na imekuwa kali na endapo mnunuzi wa pamba atajihusisha na uchezeshaji wa vipimo akakamatwa na kukuri kosa lake na kufifirishwa atatozwa faini kuanzia shilingi laki moja (100,000/=) mpaka milioni ishirini (20,000,000/=) kulingana na idadi ya makosa aliyotenda. Na endapo mtuhumiwa atakataa na kufikishwa mahakamani kwa kosa la kwanza atatozwa faini isiyopungua Shillingi 300,000/= na isiyozidi millioni 50 au kifungo kisichozidi miaka miwili (2) au vyote kwa pamoja, mujibu wa Sheria ya Vipimo sura na. 340 na mapitio yake ya mwaka 2002.
Vilevile, endapo mtuhumiwa atakamatwa na kosa kwa mara ya pili na kuendelea na akipelekwa Mahakamani akakutwa na hatia adhabu ni faini isiyopungua Shillingi 500,000/= na isiyozidi millioni 100 au kifungo kisichozidi miaka mitano (5) au vyote kwa pamoja.
Vilevile, amewataka wananchi waweze kutoa taarifa katika ofisi za wakala wa vipimo wanapokutana na changamoto mbalimbali za upimaji na pia wanaweza kutumia namba ya bure kutoa taarifa ambayo ni 0800 11 00 97.