Home Mchanganyiko BODI YA MISKITI WA IJUMAA KUMFIKISHA MAHAKAMANI DC NYAMAGANA

BODI YA MISKITI WA IJUMAA KUMFIKISHA MAHAKAMANI DC NYAMAGANA

0

*************************

NA BALTAZAR MASHAKA, MWANZA

BODI ya Wadhamini wa Msikiti wa Ijumaa jijini Mwanza inakusudia kufungua mashitaka mahakamani dhidi ya Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana (DC) Dk. Philis Nyimbi akidaiwa kumsweka mahabusu kwa saa 36 Katibu wa bodi hiyo Sheikh Abdallah Amin.

Mkuu huyo wa wilaya anadaiwa kutoa amri ya kukamatwa kwa kiongozi huyo wa dini kuwekwa mahabusu kwa madai ya kukaidi maelekezo ya kuachia madaraka yake kwa miezi mitatu na kukabidhi mali, vitendea kazi na nyaraka zote za Msikiti wa Ijumaa kwa Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (BAKWATA) Mkoa wa Mwanza.

Akizungumza na waandishi wa habari baada ya tamko la bodi hiyo jana Sherally Hussein Sherally, aliyejitambulisha kuwa ni mjumbe wa bodi ya wadhamini wa Msikiti wa Ijumaa, alisema watafungua shauri mahakamani dhidi ya DC kupinga uvujifu huo wa sheria aliodai unashikinizwa na watu wenye maslahi ya kuchukuliwa kwa mali za msikiti wao.

Alisema kitendo cha kukamatwa na kuwekwa mahabusu katibu wa bodi hiyo kwa amri ya Mkuu wa Wilaya kinalenga kuwaziba mdomo wasizidai mali za waislamu,kwamba huko ni kuchelewesha haki lakini ni lazima mali hizo zirudishwe mikononi mwa waislamu wenyewe.

Sherally alisema wanapata wasiwasi kutokana na vitisho vya mkuu huyo wa wilaya na ni wapi anapata  nguvu na kiburi kuvunja sheria za nchi kwa sababu hana haki ya kutoa amri mali za taasisi iliyopo kisheria zikabidhiwe kwenye taasisi nyingine isipokuwa Kabidhi Wasii Mkuu (RITA) kwa idhini ya mahakama.

Mwenyekiti huyo wa zamani wa msikiti huo alidai migogoro inasababishwa na wanaong’ang’ania mali za waislamu na fedha zinazotokana na vitega uchumi vya Msikiti wa Ijumaa ndizo zinazowatesa,zinavuruga amani ya Mwanza na kupotosha ukweli kuhusu mali hizo.

Alisema “Tunataka umma wa watanzania na viongozi wa serikalini ujue,tatizo na vita yetu linahusu mali za waislamu (shule ya sekondari Thaaqafa, kituo cha Afya cha Al Ijumaa na maduka) zimegeuzwa kuwa mali ya watendaji waliokabidhiwa kuzisimamia, wakati zimejengwa kwa sadaka za waumini.Fedha nyingi kutoka vyanzo hivyo ndizo zinatumika sehemu mbalimbali ili kutuvuruga na kutukandamiza. ”

Sherally na kuongeza kuwa; “Bodi ndiyo ilistahili kuwekwa ndani na si Katibu ambaye ni mteuliwa na hana mali,wenye mali ni bodi ya wadhamini ndio walitakiwa wazikabidhi.Lakini tunapata wasiwasi kukabidhi mali za msikiti wa Ijumaa, BAKWATA bila kutumia sheria.”

Mjumbe huyo wa bodi ya wadhamini alifafanua kuwa Sheria namba 14(2) na 15 (2) “The Regional Administration Act” namba 19 ya mwaka 1997 aliyotumia DC  haihamishi mali bali inampa mamlaka ya kuchukua hatua dhidi ya mtu anayevunja amani na utulivu wa umma na kuhoji Sheikhe Amin alivunja amani wapi.

“Katibu na Imamu wamekamatwa kwa amri moja, inashangaza na kusikitisha kuona Imamu Hamza Mansoor na Maruzuku Magongo wanaovunja amani, kwa kukataa makubaliano na suluhu ya kamati na kuleta wanafunzi 400 (mamluki) kufanya mapinduzi ya uongozi hawakamatwi.Pia migogoro ya kidini,lakini haikuwahi kutokea kiongozi wa serikali kuagiza mali za taasisi iliyosajiliwa kisheria kwenda taasisi nyingine kwa madai ya kulinda amani,”alisema Sherally.

Katibu wa bodi, Sheikhe Amin  alikamatwa Juni 10, mwaka huu kwa amri ya mkuu wa wilaya ya Nyamagana kwa kile alichokiita kukataa kutoshughulisha na mambo ya msikiti wa Ijumaa, kukabidhi ofisi, mali na nyaraka kwa BAKWATA mkoa ndani ya muda wa siku tatu kwa maagizo ya kamati ya ulinzi na usalama.

Alisema  barua hiyo ya maelekezo aliipokea Juni 4, mwaka huu zikiwa zimebaki siku tatu  za utekelezaji( baada ya siku 23 kupita) tangu iandikwe Mei 13, mwaka huu na kusainiwa na Katibu Tawala wa Wilaya ya Nyamagana  (DAS) Alfred Yonas.

Kwa mujibu wa Sheikhe Amin, Juni 6, mwaka huu alimwandikia DC barua yenye kumb. Na.RTJM/GEN/2019/50 akiomba ufafanuzi wa agizo lake la kukabidhi mali za taasisi iliyosajiliwa kisheria na kuipa taasisi nyingine bila idhini ya mwenye mali wala taratibu za kisheria.

Alieleza kuwa, mkuu huyo wa wilaya badala ya kujibu barua hiyo au kutoa maelekezo, aliagiza kiongozi huyo wa kidini akamatwe pasi na kujali, umri na afya yake kwa alichokiita kutokutekeleza agizo la kamati ya ulinzi na usalama ya wilaya. 

Mbali na katibu huyo mwingine ni Imamu wa Msikiti wa Raudhwa, Sheikhe Amir Kibonge ambaye naye alikamatwa Juni 9, mwaka huu na kuwekwa mahabusu kabla ya kuachiwa akidaiwa kukaidi maelekezo ya mkuu wa wilaya, yakimtaka kukabidhi BAKWATA mali za msikiti huo.

Kwa upande wao Imamu Hamza Mansoor na Maruzuku Magongo,wakizungumzia tuhuma na madai dhidi yao walisema tamko hilo lililotolewa na Abdallah Amin, si la bodi na wala hawamtambui Sherally Hussein Sherally kwani si mjumbe wa bodi ya Msikiti wa Ijumaa.

Walisema  bodi hiyo ina wajumbe saba wanaotambuliwa na serikali, kati yao wawili wamefariki dunia na hivyo mgogoro uliopo msikitini hapo unasababishwa na Katibu wa Bodi (Abdallah Amin) kutaka kuhodhi mali za msikiti.

“Katibu ana tabia ya kuzungumza kwa niaba ya bodi wakati  wajumbe hawajakutana na kumtuma kwani  kati ya wajumbe saba, wanne  hawamuungi mkono.Ananifanyia visa na kutoa taarifa za uongo serikalini, dhamira yake abaki na mwanaye ili afanye atakavyo.Hivyo wajumbe wa bodi walipaswa kukutana kabla ya kutoa tamko hilo,”alisema Imamu Mansoor.

Alidai Katibu aliswekwa mahabusu baada ya kushindwa kutekeleza wajibu wa kisheria,kukabidhi ofisi Bakwata baada ya kamati ya ulinzi na usalama ya Wilaya ya Nyamagana kuagiza pande zote zikae pembeni hadi suluhu ya mgogoro wao ipatikane ambapo Mansoor alitii lakini Abdallah Amin aligoma.

“Mgogoro wa Msikiti wa Ijumaa ni wa kugombea mali na mapato yanayotokana na vitega uchumi vya msikiti huo (maduka 200, nyumba 10 za biashara na nyumba za wakfu), si  jambo jingine.Msikiti huo umendelezwa na waumini wenyewe kwa kutoa mali na fedha zao na si mali ya familia,”alisema Magongo.

Pia Magongo alikana tuhuma za kukusanya wanafunzi 400 kuvamia msikiti ili kufanya mapinduzi ya uongozi na kumrejesha Mansoor, akisema kuwa si kweli kwa kuwa wanafunzi hawaruhusiwi kuswali nje ya shule,isipokuwa baadhi ya walimu wa madrasa walikwenda kusaidia kuorodhesha waumini wa Msikiti wa Ijumaa siku hiyo.

Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana Dk. Nyimbi Juni 19, mwaka huu mchana alipigiwa simu lakini haikupokelewa kabla ya kujibu kwa ujumbe mfupi; “Niko kwenye kikao”  ambao alitumiwa ujumbe alitumiwa ujumbe mfupi wa simu na mwandishi akiomba ufafanuzi wa malalamiko ya yaliyotolewa na viongozi wa dini ya kiislamu wa bodi ya Msikiti wa Ijumaa na Imamu wa msikiti wa Raudhwa kukamatwa na kuwaweka mahabusu hakujibu.

Hata hivyo  majira ya saa 8:56 alimpigia mwandishi wa habari hizi baada ya kujitambulisha alidai :Sijui naongea nani kwa sababu akina Baltazar wapo wengi” licha ya kufafanuliwa alisema “Niko ofisini” akakata simu”.

Majira ya saa 9:03 baada ya DC huyo kukata simu, alipopigiwa tena simu alisema yuko kwenye kikao ambapo mwandishi aliomba ahadi ya kumwona ofisini kwake Alhamis akajibu hatakuwepo, atakuwa na ratiba ya kuwaona wananchi wa wilaya yake.