Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira, Barozi Joseph Sokoine akizungumza na wanahabari wakati wa zoezi la ufanyaji usafi, katika kilele cha wiki ya utumishi wa Umma zoezi lililofanyika katika mtaa wa Makulu.
Mkuu wa Wilaya ya Dodoma Patrobas Katambi akizungumza na wananchi wa Makulu, baada kukamilika kwa zoezi la kukusanya taka ngumu na mifuko ya plastiki.
Mkuu wa Wilaya ya Dodoma Patrobas Katambi akimkabidhi bibi zawadi ya shilingi elfu hamsini, baada ya kushiriki kikamilifu katika zoezi la kuondoa mifuko ya plastiki eneo ya Makulu jijini Dodoma.
Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira, Barozi Joseph Sokoine aliyeinama akishiriki katika zoezi la kuondoa mifuko ya plastiki katika eneo la Makulu.
Baadhi ya watumishi wa Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira wakishiriki katika zoezi la kuondoa taka ngumu na mifuko ya plastiki katika eneo la Makulu jijini Dodoma.
Taka ambazo zimekusanywa wakati wa zoezi hilo.
Baadhi ya wananchi wakati wa zoezi hilo, wakimsikiliza afisa Mazingira wa Jiji la Dodoma Ally Mfinanga (hayupo pichani) alipokuwa akitoa elimu juu ya madhara ya mifuko ya plastiki wakati wakati wa zoezi hilo eneo la Makulu jijini Dodoma.
Afisa Mazingira wa Jiji la Dodoma Ally Mfinanga akitoa elimu kwa wananchi wa Makulu (hawapo pichani), juu ya madhara ya mifuko ya plastiki wakati wa zoezi hilo, lililofanyika eneo la Makulu jijini Dodoma.
Baadhi ya watumishi wa halmashauri ya Jiji la Dodoma walioshiriki katika zoezi hilo.
(PICHA NA ZOTE NA EZEKIEL NASHON)
…………………….
Na EZEKIEL NASHON, DODOMA.
KATIKA kuadhimisha siku ya wiki ya utumishi wa umma, Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira kwa kushirikiana na halmashauri ya Jiji la Dodoma wamefanya zoezi la kufanya usafi na kuondoa mifuko ya plastiki katika mtaa wa Makulu, kata ya Makulu, jijini hapa.
Akizungumza na waandishi wa habari wakati wa zoezi hilo Naibu katibu mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na mazingira, Barozi Joseph Sokoine, amesema lengo la kufanya zoezi la usafi ni kuwahamasisha wananchi kuendelea kuondoa mifuko ya plastiki kuweka maeneo safi.
“ Tumefanya zoezi hili lengo ni kuhakikisha tunawapa hamasa wananchi waendelee kusafisha mazingira yawe safi baada ya zuio mifuko bado imetapakaa sana kwahiyo hili ni kuhamashisha ili tuweke mazingira safi” amesema.
Pia amesema zoezi hilo litakuwa endelevu na kuwaomba wananchi kujenga utamaduni wa kulinda mazingira ili yawe safi kwani mazingira ni muhimu sana kwa afya ya binadamu.
Amebainisha zoezi hilo linaenda sambamba na kutoa elimu kwa wananchi madhara ya kutumia mifuko ya plastiki, vilevile kuwasaidia kuwaelimisha utumiaji wa mifuko mbadala ambayo ni salama kwa afya zao.
“Zoezi hili limeenda sambamba na kutoa elimu kwa wananchi kuachana na matumizi ya mifuko ya plastiki, pia kuwaelimisha namna ya kutumia mifuko mbadala ili kuweka safi mazingira yetu” amesema.
Amesema baada ya zoezi hilo kukamilika watatumia mda huo kupima ni kiasi gani cha mifuko ambayo imekusanywa katika eneo moja lengo ni kujua mazingira yameathirika kwa kiasi gani.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Dodoma Patrobas Katambi, mbali na kuwapongeza watumishi wa Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira kwa kushiriki katika zoezi hilo, amesema zoezi hilo linaumuhimu mkubwa sana kwani linaenda kuweka mazingira safi.
Amewaomba wananchi wa katika Wilaya hiyo kuendelea kufanya usafi ili mazingira yawe safi kwani sasa ni makao makuu ni muhimu sana kuwa safi.
“Kwakweli ni niseme zoezi hili ni zuri niwapongeze Ofisi ya Makamu wa Rais kwa zoezi hili kwani linaenaenda kuweka alama katika kuwahamasisha wananchi kuweka mazingira safi” amesema.
Amesema mifuko ya plastiki inamadhara makubwa katika mazingira ndio maana serikali ikaamua kupiga marufuku kwani mifuko iwapo katika mazingira ni hatari kwa afya na kwa viumbe hai katika mazingira.
Amesema wao kama jiji wataendelea kutoa elimu na kusimamia matumizi sahihi ya mifuko mbadala na kuendelea kuhamasisha uondoaji wa mifuko ya plastiki katika mazingira.