*************************
NA EMMANUEL MBATILO
Klabu ya Manchester United inasemekana ipo kwenye hatua za mwisho za kumsajili beki wa Crystal Palace, Aaron Wan-bissaka, ambaye wamekuwa wanamfukuzia wa muda mrefu.
Wan-Bissaka anahesabiwa kama miongoni mwa mabeki bora wa kulia kwenye Ligi Kuu England. Manchester United inasemekana imekubali kulipa ada ya pauni milioni 60 (Sh. bilioni 174) ili kumchukua WanBissaka, ambaye pia anachezea timu ya vijana ya England wenye umri wa chini ya miaka 21.
Dili baina ya Manchester United na Wan-Bissaka linatazamiwa kukamilika katika siku chache zijazo. Beki mwenyewe naye inaaminika anataka kujiunga na Manchester United.
Wan-Bissaka aling’ara na Crystal Palace katika msimu wa 2018/19 ambapo alicheza jumla ya mechi 39 katika mashindano yote. Manchester United ina tatizo la beki wa kulia, ambapo kwa kiasi kikubwa imekuwa inamtegemea beki mkongwe Ashley Young. Wan-Bissaka akitua Manchester United atakuwa mchezaji wa pili kusajiliwa na timu hiyo baada ya winga Daniel James.