Home Mchanganyiko SIKU 21 ZA KUTEMBELEA MAAJABU YA RAIS MAGUFULI

SIKU 21 ZA KUTEMBELEA MAAJABU YA RAIS MAGUFULI

0

Tukiwa safarini kwa ajili ya ziara hiyo tuliyotembelea miradi ya ujenzi wa bandari katika maziwa makuu ya Victoria, Tanganyika na Nyasa.

…………………………………………………….

HUWA sina tabia ya kusimulia mambo mengi ambayo nayashuhudia na kuyaona kwa macho yangu lakini ukweli safari hii nimeshindwa.Acha nisimulie bwana.

Simulizi yenyewe inaanzia hapa na kadri nitakavyokuwa nakumbuka nitaendelea kuielezea.Nipe muda wako ingawa najua tuko kwenye majukumu kwa kila mmoja wetu kuhakikisha Tanzania inapiga hatua kimaendeleo kupitia kauli mbiu ya Hapa Kazi Tu na ile ya Tanzania ya kuelekea uchumi wa kati kupitia Tanzania ya Viwanda.

Basi ndugu yangu Mtanzania, Juni 2 mwaka huu wa 2019 nilibahatika kuwamo kwenye orodha ya waandishi wa habari kupata fursa ya kutembelea miradi  mbalimbali inayotekelezwa na Serikali nchini chini Mamlaka za  Bandari za Maziwa Makuu ya Victoria, Tanganyika na Nyasa.

Siku hiyo nakumbuka ilikuwa  saa moja asubuhi wote tuliokuwa tunasafiri tukakusanyika eneo la Magomeni jijini Dar es Salaam, Katika safari hiyo mimi ndiyo nilikuwa naonekana mtu mzima wengine wote  walikuwa ni vijana lakini tulikuwa kitu kimoja na tulishirikiana vizuri kiasi kwamba kuna vitu nitaendelea kuvikumbuka maishani mwangu kutokana na safari hiyo.

Jina la dereva wetu ni Hassan Shaban na hivyo safari ikaanza mdogomdogo.Hata hivyo wakati tumeanza safari akili yangu ikawa ni kwenda kuona huko tunakokwenda kuna nini.

Kabla ya kuanza safari tulifanya maombi ili Mungu aweke mikono yake kwenye safari yetu kisha tukaondoka maombi hayo yakifanywa na kijana wangu wa story nyingi Humphrey Shao. Dereva akaanza kutia gia na tulipofika Chalinze tukasimama kwa ajili ya kupata kifungua kinywa a.k.a chai.

Baada ya kupata chai tukaendelea na safari yetu.Hakika dereva wetu alikuwa akizingatia sheria za usalama barabarani.Aliongeza spidi na kupunguza kulingana na alama zilizopo barabarani.Kwenye 50 alikwenda kwa spidi 50 na kwenye spidi 80 alikwenda kwa kufuata maelekezo.Hatukuwa na shaka.

Safari yetu ikawa inaendelea na ilipofika saa 12 jioni tukaingia katika Mji wa Dodoma ambako ndiko yaliko makao makuu ya nchi yetu.Hongera Rais wangu mpendwa Dk.John Magufuli kwa uamuzi wako wa kuihamishia Serikali Dodoma.Imebadilika tofauti na wakati ule.

Tulipoingia Dododma tukaenda eneo la Mwanga ambalo ni maarufu kwa vyakula na vinywaji.Tukapata chakula na baada ya hapo tulianza tena safari kigiza kikiwa kimeanza.

Tukiwa bado safarini tukashauriana tulale wapi? wengine wakasema tulale Singida, Lakini Mkuu wa Msafara huo ambaye ni Afisa Habari Mwandamizi wa Mamlaka ya Bandari (TPA) Bw. Leonard Magomba akashauri tukalale Igunga ili kupunguza umbali wa safari ili kufika Mwanza mapema ambako ilikuwa lazima tuanze kazi mchana uleule mara baada ya kufika.

Basi safari ikaendelea huku tukitaniana kwa maneno ya hapa na pale na kufurahi pamoja jambo ambalo liliifanya safari yetu kuwa nyepesi, Kuna madogo wawili mmoja anaitwa Willy na mwingine anaitwa Hirraly basi walikuwa watundu sana.

Huyu Willy alikuwa mtundu zaidi, alikuwa akiongea sana mara anacheza muziki yaani mpaka tunamwita (Prapraa) kwenye gari hata kama hutaki kucheka akiongea yeye tu gari zima lazima tutacheka.

Safari yetu usiku ule ilitufikisha Misigiri Kiomboi mkoani Singida kabla ya kushuka mlima Sekenke ambapo kuna geti la askari kwa ajili ya usalama, Tuliposimama alikuja askari polisi akatuambia hatuwezi kuvuka kuelekea Igunga kwani muda ule ulikuwa mbaya na usiku mkubwa kwani eneo la mlima Sekenke siyo salama.

Hatukuwa na jinsi Dereva wetu Hassan Shaban akaelekezwa eneo la kupaki gari kisha watu wakalala kwenye gari lakini mimi na kujana wangu Humphrey  Shayo tukaona ni vyema tutafute Gesti tujiegeshe kidogo na kuchaji simu  na vifaa vyetu vya kazi.

Ilipofika Saa 10:00 Alfajiri tuliamka tukaelekea kwenye gari ambako baadhi ya wenzetu pia walikuwa wameamka, Dereva Hassan Shanban akawasha gari na kuisogeza kwenye geti,  lakini askari wakakataa tena wakisema mpaka ifike saa 11:00 tukajaribu kuongea na mmoja wao ambaye inaonekana ndiye alikuwa msimamizi wao usku ule baadaye alikubali na kuturuhusu tukaondoka na safari.

Nilishangaa jambo moja kutoka kwa Dereva Hassan alikuwa ni mtu mpole mwenye Heshima, Nidhamu  na mwenye kuijua vyema kazi yake aliendesha gari kwa kufuata taratibu na sheria zote za usalama barabarani, wakati wote hakuonyesha kuchoka.

Akiulizwa swali na trafiki mnakwenda wapi alikuwa na jibu moja tu “Niko na waandishi wa habari wana kazi maalum hivyo tunazunguka mikoa mbalimbali kwa ajili ya kazi hiyo”.

Matrafiki walimwelewa sana na hawakutaka kuongeza swali zaidi ya kuturuhusu tuendelee na safari,  labda ni kwa namna alivyokuwa akijibu kwa Busara, Hekina, Unyenyekevu  na kutii sheria bila shuruti.

Basi tulifika Mwanza majira ya saa 8:00 hivi mchana, moja kwa moja tulienda Club Villa eneo la Furahisha jijini humo karibu na uwanja wa mpira wa Kirumba  ambako ni maarufu kwa Chakula, Vinywaji na Burudani za muziki lakini kubwa ililotupeleka hapo mchana ule lilikuwa ni kupata  Chakula  cha mchana kisha tuanzea kazi kwa sababu tulitakiwa kuonana na Kaimu Meneja wa Mamlaka  hiyo Bw. Geofrey Lwesya mchana ule.

Wengi wetu tulipata Samaki Sato na Ugali baada ya Chakula tulienda Makao Makuu ya Mamlaka ya Bandari za Ziwa Victoria (TPA) zilizoko katika Bandari ya Mwanza Kaskazini ambako tulipokelewa na Kaimu Meneja huyo.

Bw. Godfrey Lwesya alitukaribisha katika ukumbi wa mikutano wa  ofisi hizo, tulitambulishana kisha alitupa taarifa yake kwa ufupi kuhusu miradi inayotekelezwa na serikali chini ya Mamlaka ya bandari za ziwa hilo

Nikiangalia picha ya Meli ya MV Songea iliyobandikwa ukutani katika ofisi za Makao Makuu ya Bandari jijini Mwanza.

…………………………………….

Tukiwa ofisini hapo wakati nikiangalia picha mbalimbali ukutani niliona moja ya picha ambayo ilinikumbusha mbali sana, picha yenyewe ilikuwa ni ya Meli ya MV Songea iliyokuwa ikifanya safari zake katika ziwa Nyasa.

Kuna wakati niliwahi kuipanda meli hii kutoka Mbambabay wilaya ya Nyasa mkoani Ruvuma kwenda Itungi Port Kyela mkoani Mbeya tukiwa katika msafara wa Katibu Mkuu Mstaafu wa CCM wakati huo Kanali Abdulrahman Kinana.

Katika safari hiyo ya masaa 26 majini kuna wakati tulipigwa mawimbi makubwa tukapata msukosuko sana mpaka tulikosa matumaini ya kufika salama tulikokuwa tukienda.

Lakini Meli hiyo iliongozwa chini ya Kapteni Faya ambaye aliipitisha kwa shida katika eneo la mawimbi kwenye makutano ya maji ya Mto Luhuhu na ziwa Nyasa

Kwa umakini mkubwa wa kapteni yule hatimaye tulifika salama  katika bandari ya Itungi na tukapokelewa na Waziri wa Uchukuzi na Mawasiliano wakati huo Dk. Harrison Mwakyembe nakumbuka jinsi ambayo kila mmoja alikuwa akimuomba mungu ili tufike salama.

Baada ya taarifa yake Kaimu Meneja wa Mmlaka hiyo Bw. Godfery Lwesya alitupeleka Bandari ya Mwanza Kusini kujionea  baadhi ya miradi inayoendelea bandarini hapo na shughuli mbalimbali zinazofanyika

Huo ukawa ndiyo mwanzo wa safari ya kujionea maajabu ya Rais Dk.John Magufuli katika Maziwa Makuu ya Victoria, Tanganyika na Nyasa,  ambapo katika bandari ya Mwanza Kusini nikaona ujenzi wa eneo kubwa la Chelezo kwa ajili ya ujenzi wa meli mpya kubwa ya abiria na meli ya MV Victoria ikikarabatiwa …………………………………INAENDELEA

Hii ni meli ya MV Victoria ambayo inakarabatiwa katika bandari ya mwanza kusini  ina uwezo wa kubeba abiria 1200 na tani 200 za mizigo na nyingine ya MV Butiama ambazo zitakamilika mwezi Machi 2020.

ENDELEA KUFUATILIE SIMULIZI HII NITAKUSIMULIA MAAJABU YA RAIS MAGUFULI NILIYOYAONA.