Home Mchanganyiko MTENGETI AMEWATAKA WANANCHI KUTOA USHIRIKIANO KWA VYOMBO VYA USALAMA KUTOKOMEZA UKATILI WA...

MTENGETI AMEWATAKA WANANCHI KUTOA USHIRIKIANO KWA VYOMBO VYA USALAMA KUTOKOMEZA UKATILI WA KIJINSIA NA WATOTO

0

*************************

NA EMMANUEL MBATILO

Changamoto kubwa kwa Mahakama kufanya maamuzi hasa katika kesi za unyanyasaji wa kijinsia na watoto husababishwa na Jamii kutokutoa ushahidi  kutokana na mhanga wa tukio hilo hufanyiwa na ndugu yake wa karibu.

Ameyasema hayo Mkurugenzi Mkuu wa CDF Bw. Koshuma Mtengeti katika kikao cha mrejesho wa mafunzo ya Makamanda wa polisi wa Mikoa, Tanzania bara na Visiwani kwa lengo la kujua ni jinsi gani wanaweza kuboresha huduma zitolewazo na dawati la jinsia na watoto pamoja na changamoto ambazo zimekuwa zikijitokeza mara kwa mara.

“Kumekuwa na changamoto ya jinsi gani maamuzi yanafanyika katika mahakama zetu na ambazo zinasababishwa na jamii kutokutoa ushahidi na mara nyingi unakuta wahanga wa ukatili hasa watoto huwa wanafanyiwa na watu wa karibu kwahiyo inakuwa ni ngumu sana kwa familia ile kwenda kutoa ushahidi mahakamani kwa kuhofia kwamba ndugu yao anaweza kushitakiwa na kufungwa kwahiyo kuna changamoto ya kupata ushahidi ili watoto waweze kupata haki zao”. Amesema Bw.Mtengeti.

Bw.Mtengeti ameongeza kuwa nguvu zaidi inatakiwa kuwekwa katika kukuza uelewa kwa jamii kuhusu haki ya mtoto na kuwaelewesha jinsi gani wanawajibu wa kuwalinda watoto pamoja na kuwashirikisha jeshi la polisi kuhakikisha matukio yanapungua.

Kwa upande wa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya SACP.Ulrich Matei amesema kuwa jitihada wanazozifanya wao kama jeshi la polisi kupambana na matukio ya unyanyasaji hasa kwa watoto wanawake mara nyingi wanafanya vipindi vya kuelimisha hasa katika redio pamoja na makongamano kukemea ukatili kwa watoto na wanawake.

“Takwimu za kuanzia Januari mpaka Mei kumekuwa na kesi za kubaka 159 wakati kesi za kuwapa mimba wanafunzi zilikuwa kesi 112 ambazo zimekuwa tishio”. Amesema SACP. Matei.

Hata hivyo naye Kamishina Msaidizi wa Mkoa wa Manyara Agustino Senga amesema kuwa Mila na desturi pamoja na jeografia iliopo katika mkoa wa Manyara ndio chanzo cha matatizo ya Unyanyasaji wa kijinsia kuwepo.

Jeshi la polisi kushirikiana na taasisi mbalimbali tutaendelea kutoa elimu ili wafahamu baadhi ya mila potofu zimekatazwa kisheria kwani zingine ni hatari kwa afya “. Amesema ACP.Senga.

Aidha ACP.Senga ameongeza kuwa katika wilaya Babati takwimu zinaonyesha katika miezi mitatu ya mwisho kumekuwa na  kesi 120 zitokanazo na ukatili wa kijinsia.