Mkurugenzi Mtendaji wa CDF, Bw.Koshuma Mtengeti akiwa pamoja na Kamishina wa Ushirikishwaji wa Jamii CP. Mussa Ally ambaye alikuwa mgeni rasmi katika Kikao cha Mrejesho wa Mafunzo ya Makamanda wa Polisi wa Mikoa, Tanzania uliofanyika Leo jijini Dar es Salaam.
Makamanda wa Mikoa wakiwa wamehudhulia katika Kikao cha Mrejesho wa Mafunzo ya Makamanda wa Polisi wa Mikoa, Tanzania uliofanyika Leo jijini Dar es Salaam.
NA EMMANUEL MBATILO
Makamanda wa Mikoa watakiwa kuwatembelea Wananchi wao ili kuweza kutambua changamoto ambazo wanakutana nazo hasa katika masuala ya unyanyasaji.
Ameyasema hayo leo Kamishna wa Ushirikishwaji wa Jamii CP. Mussa Ally katika Kikao cha Mrejesho wa Mafunzo ya Makamanda wa Polisi wa Mikoa, Tanzania kilichofanyika Jijini Dar es Salaam.
Akizungumza na wanahabari Jijini Dar es Salaam Kamanda huyo amewataka Makamanda wote wa mkoa kuendelea na kasi ambayo mwanzo walikuwa wanionyesha ya uwajibikaji katika kazi kwenye Mikoa yao ili kuweza kuhakikisha amani kwa wananchi.
“Mkawapange askari wa kata kwa watendaji kata ili kero zinazojitokeza mara kwa mara zipungue”.
Aidha CP. Mussa amewataka makamanda wakajipange hasa katika chaguzi mbili zijazo kuhakikisha amani inakuwepo kwa wananchi kwa ujumla.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Shirika la Utu wa Mtoto CDF, Bw. Koshuma Mtengeti amesema kuwa Shirika la CDF na jeshi la polisi kupitia ufadhili wa shirika la idadi ya watu Duniani UNFPA na balozi wa Swedeni Tanzania wamefanikiwa kutoa mafunzo ya jinsi ya kushughulikia kesi za ukatili dhidi ya wanawake na watoto kwa askari polisi 270 (Wakiume 152 na wanawake 118) kutoka katika Mikoa ya Mara, Tarime/Rorya, Ilala, Dodoma, Manyara na Kigoma.
“Tumejenga na kukamilisha madawati ya jinsia na watoto (Manyovu, Uvinza na Buhigwe). Madawati 22 ya Jinsia na watoto yamepatiwa vitendea kazi, vifaa kama komputa, printa na moderm kwa ajili ya kurahisha kazi ya kukusanya taarifa za kesi za wahanga wa ukatili wa jinsia na watoto . lakini pia kuhifadhi kumbukumbu za kesi hizo kwaajili ya kutengenezea program mbalimbali za kutokomeza ukatili dhidi ya watoto na wanawake”. Amesema Bw. Mtengeti.
Ameongeza kuwa hivi karibuni timu ya CDF ikishirikiana na Jeshi la Polisi Kitengo cha Dawati la Jinsia na watoto, wamefanikiwa kupitia maeneo ambayo ujenzi wa madawati mapya kumi na moja na kituo cha Polisi cha Buhigwe. Madawati mapya ni pamoja na Bunda, Serengeti, Butiama, Simanjiro, Mererani, Mbulu, Kiteto, Hanang, Tarime na Sirari.