Rais wa Umoja wa Wanamuzi Tanzania (TAMUFO) Dkt.Donald (kushoto), akimpongeza Mbunge wa Viti Maalumu (CCM) Mkoa wa Iringa, Ritta Kabati baada ya Chuo cha Africa Graduate University cha Lusaka nchini Zambia kumtunuku Tuzo ya Heshima ya Udaktari (PhD) katika mahafali ya 37 ya chuo hicho yaliyofanyika mwishoni mwa wiki nchini Zambia.
Makamu Mkuu wa Chuo hicho chenye makao makuu yake nchini Sierra Leone, Profesa Timothy Kazembe (kushoto), Katibu Umoja wa Wanamuzi Tanzania (TAMUFO), Stellah Joel wakiwa na Mbunge Kibati baada ya kutunukiwa Tuzo hiyo.
Katibu Umoja wa Wanamuzi Tanzania (TAMUFO), Stellah Joel, akimpongeza Mbunge Kibati baada ya kutunukiwa Tuzo hiyo. |
Na Dotto Mwaibale
CHUO cha Africa Graduate University cha Lusaka nchini Zambia kimemtunuku Tuzo ya Heshima ya Udaktari (PhD) Mbunge wa Viti Maalumu (CCM) Mkoa wa Iringa Ritta Kabati pamoja na Tanzania wengine wanne.
Waliotunukiwa tuzo hizo za heshima ni wale waliotoa mchango mkubwa kwa kufanya shughuli mbalimbali za kujitolea za kijamii na zikaleta manufaa kwa mtu mmoja mmoja na taifa kwa ujumla.
Akizungumza mwishoni mwa wiki kwa njia ya simu wakati wa mahafali ya 37 ya chuo hicho, Makamu Mkuu wa Chuo hicho chenye makao makuu yake nchini Sierra Leone, Profesa Timothy Kazembe, alisema kila mwaka kimekuwa kikitoa Tuzo za heshima na Shahada za Uzamili kwa watanzania waliotoa mchango wa kusaidia jamii katika shughuli mbalimbali.
“Tunao watunuku tuzo hizi tuzo za heshima ni watu waliokuwa na umri wa miaka 60 ambao wanafanya kazi za kijamii katika nyumba za ibada kwa zaidi ya miaka 15 na kuendelea na wale ambao umri wao ni miaka 40 hadi zaidi na wenye shahada” alisema Profesa Kazembe.
Mbunge Ritta Kabati ametunukiwa Tuzo hiyo kutokana na mchango wake mkubwa wa kufanya shughuli mbalimbali za kujitolea za kijamii pamoja na kusaidia watu wenye ulemavu.
Wengine Waliotunukiwa tuzo ya heshima ya udaktari ni Bishop Dkt. Daniel Kwiyeya wa Zanzibar, Mhandisi Dkt.Elina Kayanga wa Tarula Dodoma, Dkt.William Henry wa Tanga pamoja na Dkt.Ester Sollo ambaye ni mwanaharakati wa kusaidia vikundi mbalimbali vya wanawake.
Baadhi ya watanzania wengine waliowahi kutunukiwa Tuzo na chuo hicho ni Askofu Dkt. Godfrey Mallasy, Ofisa wa Jeshi la Polisi Dkt. Ezekiel Kyogo, Mtakwimu Dkt. Margaret Mutaleba, Mwanahabari Dkt. Tumaini Msowoya, Mwanaharakati wa Haki za Watoto ambaye ni Rais wa Tanzania Music Foundation Dkt.Donald Kisanga, Dkt.Mlute Nyasa, Dkt.John Pallangyo,Dkt.Wilson Nyiti na Dkt.Godwin Maimu.