Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa TAMISEMI, Seleman Jafo, akiwa na viongozi wa halmashauri ya wilaya ya Kongwa katika ziara ya kutembelea miradi inayotekelezwa katika wilaya hiyo.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa TAMISEMI, Seleman Jafo, akisisitiza jambo kwa viongozi wa halmashauri ya wilaya ya Kongwa wakati wa ziara ya kutembelea miradi katika wilaya hiyo.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa TAMISEMI, Seleman Jafo, akiongea na fundi wa kufyatua tofali za block, katika hospitali ya wilaya ya Kongwa tofali ambazo zitatumika katika upanuzi wa hospitali hiyo.
Mkuu wa wilaya ya Kongwa Deogratus Ndejembi, akifafanua jambo kwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa TAMISEMI, Seleman Jafo, wakati wa ziara ya kutembelea miradi inayotekelezwa katika wilaya hiyo.
Mganga mkuu wa hospitali ya wilaya ya Kongwa Magreth Kagashe, akitoa taarifa ya utekelezaji wa upanuzi wa hospitali hiyo kwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa TAMISEMI, Seleman Jafo, alipotembelea hospitali hiyo wakati wa ziara yake.
(PICHA ZOTE NA EZEKIEL NASHON)
………………………..
Na EZEKIEL NASHON, KONGWA.
WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mtaa, TAMISEMI, Seleman Jafo, ameagiza afisa elimu Sekondari Wilaya ya Kongwa, Nelson Milanzi, kurudi toka alikokwenda kwenye mashindano ya UMISETA Mtwara, kuja kijieleza kwanini kakwamisha ujenzi wa miondombinu ya shule Wilayani hapo.
Jafo ametoa kauli hiyo Wilayani Kongwa wakati wa ziara ya kukagua miradi iliyochini ya ofisi yake, baada ya kukuta ujenzi wa madarasa, mabweni na bwalo katika shule za sekondari Sejeli na Kongwa, yakiwa katika hatua za awali wakati fedha ziliingia tangu mwezi wa kwanza mwaka huu.
Amesema apewe taarifa leo alejee katika kituo chake cha kazi na aandike barua ya kujieleza kwa katibu mkuu wa TAMISEMI kujieleza sababu za kuwa kizuizi kuto kukamilika kwa majengo hayo mpaka sasa.
Amefikia uamuzi huo baada ya kupokea taarifa kutoka kwa mkurugenzi wa halmashauri ya Kongwa Omari Mkullo kuwa kulikuwa na mvutano baina ya halmashauri na idara ya elimu sekondari mfumo wa kujenga majengo hayo.
Halmashauri ikitaka kutumia fosi akaunti huku idara ya elimu ikitaka itangazwe tenda katika kujenga majengo hayo hali iliyosababisha mkuu wa wilaya hiyo Deogratus Ndejembi kutumia nguvu kuanza ujenzi.
“Nikuagize mkurugenzi mpigie simu afisa elimu kutoka huko aliko kesho(leo) arejee na kuandika barua kwa katibu mkuu wa TAMISEMI ya kwanini kachelewesha ujenzi huu katibu mkuu ataamua maana kuna kazi nyingi za kufanya ikionekana kikwazo yeye atapangiwa kazi nyingine” amesema Jafo.
Aidha amekasilishwa kwa kuanza kufanya kazi katika miradi hiyo baada ya kusikia waziri anakwenda, amepiga marufuku tabia ya kufanya kazi kwa kusukumwa amesema hafurahishwi na hiyo tabia.
Pia ameagiza wataalamu wa ujenzi wa mkoa kwenda Kongwa kwenda kusimamia ujenzi wa miradi iliyopo katika wilaya hiyo ambayo inasuasua ujenzi wake na kuagiza mpaka tarehe 30, mwezi wa nane iwe imekamilika yote na imeanza kutumika.
“Nashangaa fedha imeingia tangu mwezi wa kwanza lakini mpaka sasa mwezi wa sita ujenzi bado kabisa, sasa namuagiza msimamizi wa ujenzi wa mkoa wa Dodoma aje kusimamia ujenzi huu ifikapo mwezi wa nane tarehe 30 ujenzi uwe umekamilika” amesema Jafo.
Ametaka miradi inayokamilika kuhakikisha inafanya kazi amesema serikali imekuwa ikiwekeza fedha nyingi sana katika miradi hii lakini haifanyi kazi na kuwataka miradi yote wahakikishe inafanya kazi.
“Kuna mradi wa soko pale Bwigiri Chamwino umekamilika lakini haufanyi kazi tumeufungua umefanya kazi wiki moja umesimama, ndugu zangu serikali inawekeza fedha nyingi sana kwenye hii miradi lengo ifanye kazi simamieni kikamilifu” amesema.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa halmashauri ya wilaya ya Kongwa Omar Mkullo, amesema miradi mingi alisimama kwa sababu kulikuwa na mvutano baina ya halmashauri na idara ya elimu namna ya kuendesha ujenzi huo.
Amesema amekuwa akiandika barua mara nyingi katika idara ya elimu lakini hazijibiwi hivyo kuchelewesha kuendelea na miradi hiyo.
Katika ziara hiyo waziri Jafo alikagua ujenzi wa machinjio ya kuku kongwa, ujenzi wa kiwanda cha maziwa, ujenzi wa mabweni, bwalo na madarasa katika shule za sekondari Sejeli na Kongwa, upanuzi wa hospitali ya wilaya na kituo cha afya ugogoni.