Home Mchanganyiko UJENZI WA MELI MPYA YA ABIRIA MV MBEYA II KATIKA ZIWA NYASA...

UJENZI WA MELI MPYA YA ABIRIA MV MBEYA II KATIKA ZIWA NYASA WAFIKIA ASILIMIA 82, AWAMU YA TANO NI VITENDO TU

0

Ujenzi wa Meli ya MV Mbeya II ambayo itakuwa na uwezo wa kubeba abiria 200 na tani 200 za mizigo umefikia asilimia 82na unatarajiwa kukamilika ifikapo Juni mwaka huu.

Akizungumza na waandishi wa habari Meneja wa Bandari (TPA) Kanda ya ziwa Nyasa Bw. Abeid Galus amesema kazi inayoendelea kwa sasa ni Kufunga mitambo, Kuweka Vyumba, Kufunga viti, na umaliziaji yaani (Finishing)

Ameongeza kwamba meli ya MV. Mbeya II itakapokamilika itaondoa kabisa adha ya abiria ambao wamekuwa wakipata tabu sana kusafiri tangu meli ndogo ya MV Songea iliposimama kutoa huduma katika ziwa Nyasa kutokana na kutokuwa katika hali nzuri.

MV. Mbeya II itatoa huduma katika bandari zote za mwambao wa ziwa Nyasa ikiwa ni pamoja na nchi jirani za Malawi na Msumbiji, hivyo kurahisisha shughuli za wafanyabiashara mbalimbali wanaosafiri na kusafirisha mizigo yao kwenda na kutoka maeneo mbalimbali ya mwambao wa ziwa Nyasa.

Meli ya MV Mbeya II inaudwa baada ya meli ya mwanzo ya MV Mbeya I kuzama mwaka 1975 eneo la Makonde wakati ilipokuwa ikifanya safari zake za kawaida katika ziwa hilo.

Ujenzi wa meli hii ni muendelezo wa serikali ya Jamhuri ya Muungano ya Tanzania chini ya Rais Dkt. John Pombe Magufuli kutatua changamoto ya vyombo vya usafiri wa majini, baada kukamilisha ujenzi wa meli mbili za awali MV Ruvuma na MV Njombe kwa ajili ya kusafirisha shehena ambapo tayari zimeanza kutoa ajira za moja kwa moja kwa wakazi wanaozungukwa na bandari hizo.

Aidha Galus amesema  Mamlaka ya Bandari inaendelea na utekelezaji wa miradi mbalimbali ya ukarabati na utengezaji wa bandari kumi na tano za ziwa Nyasa zinazopatikana katika mikoa ya Mbeya,Ruvuma na Njombe.

Galus amesema katika miradi inayoendelea kujengwa ni pamoja na ujenzi baraza ngumu eneo la kuhifadhia mizigo ya makaa ya mawe katika bandari ya Kiwira wilayani Kyela.

Kwa upande wake Nahoda wa meli ya MV Ruvuma Charles Mkumbi amesema meli hizo zimewekwa vifaa maalumu vinavyoweza kuongoza safari hivyo kuhakikisha usalama wa safari.

Wastani wa Mapato ya mwaka kwa sasa kwenye bandari za ziwa nyasa ni takribani shilingi milioni mia tatu huku ikitarajiwa baada ya miradi ya ujenzi na ukarabati wa bandari hizo kukamilika mapato yataongezeka mara kumi zaidi.

Meneja wa Bandari (TPA) Kanda ya ziwa Nyasa Bw. Abeid Galus akizungumza na Afisa Mawasiliano Mwandamizi wa Mamlaka ya Bandari TPA Bw. Leonard Magomba wakati waandishi wa habari walipotembelea na kujionea ujenzi wa meli ya MV Mbeya II katika bandari ya Itungi Kyela mkoani Mbeya.

Picha mbalimbali zikionyesha meli ya MV Mbeya II ikiendelea kujengwa katika bandari ya Itungi Kyela mkoani Mbeya.

Nahoda wa meli ya MV Ruvuma Charles Mkumbi akieleza  kwa waandishi wa habari mambo mbalimbali kuhusu meli ya MV Ruvuma.

Meli za MV Njombe na MV Ruvuma  zinavyoonekana kwa juu.

Meneja wa Bandari (TPA) Kanda ya ziwa Nyasa Bw. Abeid Galus akifafanua jambo kwa waandishi wa habari huku akionyesha meli ya MV Ruvuma.

Moja ya mashine Mya iliyopo Bandarini hapo kwa ajili ya kupakuwa mizigo kwenye meli.

Meneja wa Bandari (TPA) Kanda ya ziwa Nyasa Bw. Abeid Galus akizungumza na mabaharia wa meli ya MV Ruvuma.