***************************
Tume ya Taifa ya Uchaguzi NEC imevitaka vyama vya Siasa Nchini kufuata taratibu na sheria kwa kuwasilisha malalamiko yao kwenye tume hiyo pale inapobainika ukiukwaji wake hususan nyakati za uchaguzi.
Tume hiyo imevitaka vyama hivyo kuacha kulalamikia kwenye vyombo vya habari
ambavyo vitaishia kuandika na kutangaza habari zao tu na sio kuchukua hatua stahiki za kutatua changamoto za uchaguzi.
Hayo yamebainishwa na Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi NEC Jaji
Semistocles Kaijage Jijini Dar Es Salaam wakati akizungumza na Viongozi wa Dini
mbalimbali Nchini kuhusiana na uboreshaji wa Daftari la kudumu la wapiga kura.
Awamu ya kwanza ya uboreshaji wa Daftari la kudumu la Wapiga kura litafanyika
nchini kote mapema mwezi Julai Mwaka huu kwa ajili ya maandalizi ya chaguzi za
Serikali za mitaa ambapo jumla ya vituo Vituo 37,814 katika mikoa 31 vitahusika na zoezi hilo.
Kaijage alisema malalamiko mengi ya Viongozi wa vyama vya siasa hayajawafikia
ofisini kwao bali wanaishia kuyaona tu kwenye vyombo vya Habari suala ambalo
haliwezi kufanyiwa kazi na tume hiyo na kubainisha kuwa ni kesi moja tu ya uchaguzi iliyowafikia katika ngazi ya Taifa tangu mwaka 2006.
“Mnajua ndugu zangu viongozi wa Dini suala la malalamiko ya vyama vya siasa kuhusu uchaguzi ni suala linalohitaji kuangaliwa sana na hawa wanasiasa, mtu ana tatizo anakimbilia kwenye vyombo vya habari badala ya kuja kwetu, hatufanyi kazi hivyo,wanatakiwa kuja NEC ili tuyafanyie kazi malalamiko yao”alisema Jaji Kaijage.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Tume hiyo Dkt Athumani Kihamia aliwataka viongozi hao kutoa ushirikiano katika uboreshaji wa Daftari hilo ili liweze kuwafikia wananchi wengi zaidi.
“Tunawategemea sana nyinyi Viongozi wa Dini katika kuhamasisha wananchi
kujiandikisha katika Daftari hili, nyinyi mna watu wengi,hivyo ni rahisi kuwashawishi kutekeleza jambo hili muhimu kwa Taifa letu”alisema Dkt Kihamia.
Nae Kamishna wa Tume hiyo Jaji Maryrose Longway aliwaomba Viongozi hao wa Dini kuwasihi wanasiasa kuepukana na lawama ambayo haitawasaidia na badala yake wafuate sharia za uchaguzi.
Mwenyekiti wa Baraza kuu la Jumuiya na Taasisi za Kiislamu Tanzania Sheikh Mussa Kundecha na Mchungaji Charles Mzinga wa Kanisa la Kiinjili la Kirutheli Tanzania KKKT wameiomba Tume hiyo kutoa elimu mara kwa mara kwa jamii kuhusu umuhimu wa kupiga kura pamoja na kujiandikisha katika Daftari la kudumu la wapiga kura.