Mbunge wa jimbo la Simanjiro mkoani Manyara, James Ole Millya akizungumza juu ya upendo na kuondokana na makundi na ubaguzi ili lengo la kuwa na Simanjiro moja yenye amani na kutobaguana itimie.
Mbunge wa Jimbo la Simanjiro Mkoani Manyara, James Ole Millya akisalimiana na wananchi wa Kijiji cha Sukuro alipotembelea eneo hilo.
Mbunge wa jimbo la Simanjiro Mkoani Manyara, James Ole Millya akisalimiana na wananchi wa kijiji cha Kitiangare.
*****************************
MBUNGE wa Jimbo la Simanjiro Mkoani Manyara, James Ole Millya amewashukuru wananchi wa Vijiji vya Sukuro na Kitiangare waliomaliza mgogoro wao uliodumu zaidi ya miaka 20 wakigombea Kitongoji cha Katikati.
Mgogoro huo ulishasababisha mtafaruku mkubwa baina ya aliyekuwa mkuu wa mkoa huo Henry Shekifu na aliyekuwa mbunge wa jimbo hilo Christopher Ole Sendeka mwaka 2010.
Ole Millya akizungumza na wananchi wa kijiji cha Sukuro na Kitiangare aliwapongeza wananchi wa vijiji hivyo viwili kwa kuridhia kwa pamoja na kuachana na malumbano na mgogoro usiokuwa na tija kwao.
Alisema katika mgogoro huo yeye binafsi alikaa pembeni bila kupendelea kijiji chochote kwani vyote viwili ni vya kwake hivyo hakupaswa kupendelea kimoja aliwaachia wataalamu wagawe vitongoji kama sheria inavyoelekeza.
“Nawapongeza sana wananchi wa vijiji vya Kitiangare na Sukuro kwani hali ya amani haikuwepo lakini sasa mmemaliza mgogoro wenu na kuridhia kwa pamoja kuishi kama ndugu kwani mlikuwa kijiji kimoja kabla ya kugawanywa,” alisema Ole Millya.
Alisema hivi sasa hali ya amani na upendo imerejea baina ya vijiji hivyo viwili kama awali na wananchi wanasalimiana kwa furaha, wanaoleana na kunywa maji pamoja.
Alisema kupitia mfuko wa jimbo anatoa sh6 milioni kwa vikundi vya wanawake wa vijiji vyote viwili na sh4 kwa mradi wa maji kijiji cha Sukuro na darasa la shule ya kijiji cha Kitiangare.
Mkazi wa kijiji cha Sukuro, Lengai Ole Makoo alipongeza hatua ya kumalizika kwa mgogoro huo usiokuwa na tija uliosababishwa na baadhi ya wanasiasa wa wilaya hiyo.
Ole Makoo alisema kijiji cha Sukuro kimebakiwa na vitongoji vyake vitano na kijiji cha Kitiangare kimebaki na vitongoji vyake viwili kama ambavyo kanuni, taratibu na sheria zilivyofuatwa wakati kijiji mama cha Sukuro kilipogawanywa.
“Kijiji cha Sukuro kimebaki na vitongoji vya Katikati, Lembutwa, Lenjani, Mouwara na Lasepa na Kitiangare imebaki na vitongoji vya Loongung na Kitiangare,” alisema.
Hivi karibuni mkuu wa mkoa wa Manyara, Alexander Mnyeti alimpa onyo Mwenyekiti wa CCM wa wilaya hiyo Awadhi Omary na baadhi ya wanasiasa juu ya kutumika kwa maslahi yao katika mgogoro huo.