Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Simanjiro Bw. Yefred Myenzi, akizungumza na wandishi wa Habari ofisini kwake kuhusu kilimo cha umwagiliaji. pamoja na mambo mengine kinavyochangia katika pato la Halmashauri hiyo pamoja na kubadilisha Maisha ya wananchi wa Wilaya hiyo.
……………….
NA; MWANDISHI MAALUM – SIMANJIRO
IMEELEZWA kuwa kilimo cha umwagiliaji ni chanzo kikubwa cha mapato katika Halmashauri ya Wilaya ya Simanjiro kwani huingiza shilingi Milioni mia moja ishirini (120) hadi milioni miambili (200) kwa mwaka na kuinua pato la wananchi wilayani humo.
Hayo yamesemwa leo na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo Bwana Yefred Myenzi ambapo amesema serikali ilitoa kiasi cha takribani shilingi Bilioni 2.2 kwa ajili ya ujenzi na maboresho ya skimu zaa umwagiliaji sambamba na kuwawezesha wakulima kupata elimu ya kilimo, uendeshaji na matunzo ya miundombinu ya umwagiliaji jambo ambalo limepelekea wanachi kujikita zaidi kwenye kilimo cha umwagiliaji na kuongeza pato la Halmashauri,
“Mazao mengi yanayolimwa katika skimu za umwagiliaji ni mpunga na mazao menginge ya Mboga mboga, lakini pia kuna mazao ambayo hayalimwi katika skimu hizo kama vile Matama, Uwele na Shayiri zao ambalo linatumika kama malighafi katika viwanda vingi vya beer nchini.” Alisema Bw. Myenzi
Bw. Myenzi alisema kuwa Skimu hizo zimesaidia kuwepo na chakula cha kutosha na Usalama wa chakula katika Wilaya hiyo, Pamoja na kwamba Kilimo hicho kinakabiliwa na changamoto mbali mbali ikiwa na pamoja na skimu hizo kuwa mbali na masoko jambo ambalo linapelekea kupanda kwa gharama za usafishaji wa mazao kwenda kwenye masoko na kukosekana kwa bei ya uhakika kitendo ambacho kinamuumiza mkulima pamoja na kukosekana kwa vinu vya kuchakata nafaka jambo ambalo linapelekea kukosekana kwa chakula cha mifugo kitokanacho na mabaki ya nafaka hizo.
Awali akiongea katika kikao hicho kabla ya kutembelea skimu hizo za umwagiliaji, Mhandisi wa kanda ya Umwagiliaji Dodoma inayohusisha mikoa ya Dodoma, Singida na Simanjiro Bi Lucy Lema, alisema kuwa kutokana na kilimo cha umwagiliaji kuwa chenye tija kwa kuongeza pato la taifa na kuwepo kwa uhakika wa chakula nchini, Serikali ina mikakati kabambe ya kuendeleza kilimo hicho kwa kufanya upanuzi wa maeneo na kufanya tafiti kabla ya ujenzi wa mabwawa, kufanyia ukarabati wa Miundombinu ya umwagiliaji na kuendeleza skimu ndogo ndogo za umwagiliaji kupitia miradi mbali mbali.