Diwani wa Kata ya Loiborsiret Wilayani Simanjiro Mkoani Manyara, Ezekiel Lesenga (Mardad) akizungumzia manyanyaso wanayopata wafugaji wa Kijiji cha Kimotorok.
Baadhi ya wafugaji wa Mkoa wa Manyara, wanaolalamikia wafugaji kunyanyaswa sababu ya mifugo yao.
……………….
WAFUGAJI wa Kijiji cha Kimotorok Kata ya Loiborsiret Wilayani Simanjiro Mkoani Manyara, wamelalamikia kitendo cha maofisa wa pori la akiba la Mkungunero kukusanya ng’ombe zaidi ya 2,000 na kuchukua picha ili ionekane wamekiuka agizo la kuingiza mifugo kwenye pori hilo.
Diwani wa kata ya Loiborsiret, Ezekiel Lesenga (Mardad) akizungumza na waandishi wa habari alisema wanalaani vikali kitendo hicho cha watumishi wa Mkungunero.
Lesenga alisema japokuwa ng’ombe hizo zaidi ya 2,000 hazikuchukuliwa na Mkungunero lakini vijana wanaochunga mifugo hiyo walipata hofu na kulikimbia eneo hilo.
Alisema kitendo cha baadhi ya watumishi wa Mkungunero kukusanya mifugo yao mbugani katika sehemu ambayo siyo hifadhi ni kosa kubwa kwani wanahofia kufanyiwa hujuma.
Alisema kitendo hicho kinataka kiwachonganishe wafugaji kwa serikali ili waonekane wanakiuka utaratibu wa agizo la Wizari ya Mifugo la kutoingiza mifugo hifadhini.
“Sisi tunamuunga mkono Rais John Magufuli ambaye amekuwa akiwasemea na kuwatetea wafugaji hivyo hatuwezi kuingiza mifugo yetu hifadhini kwa hiyo tunalaani vikali kitendo hicho,” alisema Lesenga.
Alisema wanatoa tahadhari kwa serikali kwani wao hawahusiki japo watu wachache wa Mkungunero wamekusanya mifugo hiyo ili wafugaji waonekane wamekiuka agizo la serikali.
“Tunamuomba mkuu wa mkoa wa Manyara Alexander Mnyeti asikie kilio hiki cha wafugaji kwani tunataka kuhujumiwa na watumishi wachache wa Mkungunero wenye nia ovu,” alisema Lesenga.
Hata hivyo, meneja wa pori la akiba la Mkungunero, Khadija Malongo alikanusha vikali kutaka kufanyika hujuma kwa wafugaji wa eneo hilo la Kimotorok.
Malongo alisema bado wafugaji wa eneo hilo wanaingiza mifugo yao na kuchungia kwenye pori la akiba la Mkungunero.
Alisema wao wanafanya kazi kwa mujibu wa sheria, ila wafugaji wa kijiji cha Kimotorok bado wanaingiza mifugo yao kwenye pori la akiba la Mkungunero, japokuwa wamekuwa wakiwapa elimu ya kuzingatia hilo.