Mtaalam wa Tiba Radiolojia (Interventional Radiology) wa Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), Dkt. Erick Mbuguje (mwenye kofia ya bluu) na wenzake wa MNH wakifuatilia jinsi mtaalam wa Tiba Radiolojia kutoka Marekani, Dkt. Michelle Maneeveseanavyomwekea mgonjwa wa figo mpira maalum kwenye mshipa mkubwa wa damu (permanent catheter insertions) ambao unamsaidia mgonjwa kusafisha damu (renal dialysis).
…………………
Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) imeanzisha huduma mpya ya kutibu uvimbe kwenye kizazi (uterine fibroids) kwa kutumia njia ya kisasa yaTiba Radiolojia (interventional radiology).
Pia, MNH imeanzisha huduma mpya nyingine ya kuweka mipira maalum kwenye mshipa mkubwa wa damu (permanent catheter insertions) kwawagonjwa wa figo ambao wapo kwenye mfumo wa kusafisha damu (renal dialysis) au kwa wagonjwa wanaopatiwa tiba ya saratani.
Wataalam wa MNH kwa kushirikiana na Chuo Kikuu cha Yale na vyuo shiriki (kama Emory, Dartmouth) vya nchini Marekani wako kwenye programu maalum ya mafunzo ya tiba Radiolojia tangu Octoba mwaka 2018 hospitalini hapa.
Akizungumza na waandishi wa habari leo, Daktari Bingwa wa Tiba Radiolojia wa MNH, Dkt. Flora Lwakatare amesema mgonjwa mwenye uvimbe kwenye kizazi anaingiziwa mpira wenye chembechembe maalum kwenye mishipa ya damu na kwenda kuziba mishipa inayopeleka damu kwenye uvimbe.
“Baada ya mishipa kuziba uvimbe unakosa damu au chakula chake na hivyo kusinyaa na kufa kabisa. Hivyo basi mama mwenye uvimbe kwenye kizazi endapo anapatiwa tiba hii hakuna haja ya kumfanyia upasuaji kubwa wa kuondoa uvimbe,” amesema Dkt. Lwakatare.
Dkt Lwakatare amesema faida ya kutumia njia hii ya kisasa, inamsaidia mgonjwa kutofanyiwa upasuaji mkubwa na pia inampunguzia gharama za matibabu na kuondoa hatari yoyote kwa mgonjwa aliyefanyiwa upasuaji mkubwa.
Akizungumzia huduma nyingine ya kuweka mipira maalum kwenye mshipa mkubwa wa damukwawagonjwa wanaosumbuliwa na figo, Dkt Lwakatare amesema huduma hii inawanufaisha wagonjwa wa figo ambao wako kwenye mfumo wa kusafisha damu (renal dialysis) au wanaopatiwa tiba ya saratani.
Amesema tiba hii inaondoa usumbufu wa kutumia mishipa midogo ya mikononi ambayo mara nyingi ni ngumu kupatikana hasa kama inatumika mara kwa mara na kwa muda mrefu.
“Tiba hii inafaida kubwa kwa kuwa inawezesha kuepeuka upasuaji mkubwa ambao una vihatarishi (risk), kuepeuka mgonjwa kukaa hopsitali kwa muda mrefu na wanaofanyiwa tiba radiolojia mara nyingi wanaweza kurudi nyumbani siku hiyo hiyo, hivyo inapunguza gharama kwa mgonjwa na Hospitali kwa ujumla,” amesema.
Hivyo kujengewa uwezo kwa watalaam wa ndani itasadia kwa kiwango kikubwa kukuza huduma hii hapa nchini ambapo watalaam kutoka Hospitali za hapa nchini watapata fursa ya kujifunza kwa gharama nafuu na kuongeza idadi ya watoa huduma mikoani.
Naye Daktari Bingwa wa Tiba Radiolojia wa Hospitali ya Chuo Kikuu cha Emory nchini Marekani, Dkt. Janice Newsome amesema tiba radiolojia inahitaji ubunifu na kutoa huduma kwa kushirikiana.
Dkt. Janice Newsome amesema wametoa mafunzo ya kutoa huduma ya tiba radiolojia kwa wataalam wa MNH na kwamba wao wamejifunza mambo mbalimbali kupitia wataalam wetu.
“Kuwekeza kwa wataalam ni jambo muhimu na zuri kwa kuwa kazi ya kutoa huduma inahitaji kushirikiana,” amesema Dkt. Newsome.
Katika mafunzo haya ya awamu ya nne, wataalam 13 wa MNH wakiwamo madaktari, wauguzi na mafundi sanifu wamepatiwa mafunzo sambamba na kutoa huduma ya matibabu kwa wagonjwa mbalimbali.
Mafunzo na huduma za tiba radiolojia zinazotolewa MNH ni mfululizo wa programu mbalimbali za tiba radiolojia yayolianza Novemba 2017 ili kujenga uwezo kwa wataalam wa MNH. Tangu kuanzishwa kwa huduma hii, wagonjwa 339 wamepatiwa huduma ya kibingwa ya tiba radiolojia na wengi ni wagonjwa wenye uvimbe kinywani.