Mwonekano wa Mtambo wa Umeme Jua wa kusukuma maji katika Mradi wa Maji wa Heru Juu, Kasulu, Kigoma uliogharimu shilingi bilioni 1.1. Mradi huu uliotekelezwa katika Serikali ya Awamu ya Tano unahudumia wakazi 24,000.
Mnufaika akiteka maji bombani, yatokanayo na Mradi wa Maji wa Heru Juu, Kasulu, Kigoma uliogharimu shilingi bilioni 1.1. Mradi huu uliotekelezwa katika Serikali ya Awamu ya Tano unahudumia wakazi 24,000.
Mkazi wa Kijiji cha Heru Juu wilayani Kasulu Mkoa wa Kigoma akiwa amebeba ndoo ya maji aliyoyateka katika bomba la Mradi wa Maji wa Heru Juu, Kasulu, Kigoma uliogharimu shilingi bilioni 1.1. Mradi huu uliotekelezwa katika Serikali ya Awamu ya Tano unahudumia wakazi 24,000.
Picha na Abubakar Kafumba- MAELEZO
…………………….
Na Jonas Kamaleki- MAELEZO, Dodoma
Utoaji wa maji safi na salama kwa watanzania ifikapo 2020 ni moja ya vipaumbele vya Serikali ya Awamu ya Tano kwa wananchi, kipaumbele hicho kimetekelezwa kwa kiwango kikubwa Wilayani Kasulu, Mkoani Kigoma.
Kwa muda mrefu tangu Tanganyika kupata uhuru takriban miaka 58 iliyopita, wakazi wa Heru Juu, Wilayani Kasulu, Mkoa wa Kigoma hawakuwahi kupata maji ya bomba. Ni Serikali ya Awamu ya Tano ambayo imefanya juhudi za makusudi kufanya uwekezaji mkubwa wa mradi wa maji ambao umeondoa adha yaupatikanaji wa maji safi na salama kwa wakazi wa maeneo hayo.
Mradi huo wa maji umewezakuwasogezea huduma hiyo kwa wastani wa mita 5 hadi 400 ikilinganishwa na kilomita 3 hadi 5 kabla ya mradi huo. Hayo yamebainishwa na ziara ya kutembelea miradi ya maendeleo inayotekelezwa na Serikali, iliyofanywa na Maafisa wa Idara ya Habari (MAELEZO) hivi karibuni.
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji
Kasulu, Fatina Laay anasema kuwa Wilaya ya Kasulu ilikuwa na shida ya maji ambayo ilileta adha kubwa kwa akina mama na kuongeza kuwa Mradi wa Maji wa Heru Juu umetatua changamoto hiyo kwa wakazi wa eneo hilo.
Mhandisi wa Maji wa Halmashauri ya Mji wa Kasulu, Emmanuel Alexander Konkomo anafafanua kuwa mradi huo unawanufaisha wakazi zaidi ya 24,000 na maji yanapatikana saa 24.
“Ndoo moja ya lita 20 kabla ya mradi huu ilikuwa inauzwa shilingi 300, kwa sasa baada ya mradi kukamilika, ndoo hiyo inauzwa kwa shilingi 6 tu (sita), ambao ni unafuu mkubwa kwa wananchi, kwa kweli tunaishukuru Serikali ya Awamu ya Tano kwa kuwajali wananchi wake”, alisema Mhandisi Konkomo.
Kabla ya mradi huo wakazi wa Heru juu walikuwa wakitumia kati ya saa tatu hadi nne kufuata maji makorongoni, jambo ambalo lilikuwa likileta usumbufu mkubwa kwa akina mama na kuwasababishia kushindwa kufanya shughuli nyingine za uzalishaji mali kwani muda mwingi ulikuwa ukitumika kwa kuteka maji.
“Tulikuwa tunaamka usiku ili tuweze kuwahi kuteka maji makorongoni ambapo ilibidi tutembee kama kilometa nne na zaidi kupata ndoo moja ya maji, kwa kweli tunamshukuru sana Mhe. Rais John Pombe Magufuli kwa kutukumbuka sisi wanyonge ambao tulikuwa tunateseka sana kutafuta maji”, anasema Consolata Sigwejo, Mkazi wa Heru Juu.
Mradi huu wa maji unatumia umeme jua katika kuyatoa maji kwenye chanzo na kuyapandisha kwenye matenki ambayo yako kwenye vilima kwa ajili ya kusambaza maji kwa wakazi wa maeneo husika.
Usambazaji wa maji hayo unafanyika kwa njia ya mserereko( gravity), jambo ambalo linafanya bei ya maji kwa mtumiaji kuwa nafuu.
Hizi zote ni juhudi za Serikali ya Awamu ya Tano katika kutimiza na kutekeleza ahadi yake ya kuwapatia wananchi maji safi na salama.
Kwa mujibu wa Mhandisi Konkomo, jumla ya wakazi 173 wameunganishiwa maji majumbani kwao na hivyo kuondokana kabisa na adha ya upatikanji wa maji iliyokuwepo kabla ya mradi huo.
Aidha, Mhandisi Konkomo anasema kuwa katika Kata ya Heru Juu, jumla ya vituo 52 vimejengwa kwa ajili ya kutolea huduma ya maji kwa wakazi wa maeneo hayo.
Meneja wa Mradi wa Maji, Heru Juu, Kwigize Venance Kahagaze anasema Mradi huu una kikundi cha kusimamia na kutunza mazingira ambacho shughuli moja kuu ni kutunza chanzo cha maji kwa kupanda miti na kuzuia shughuli za kibinadamu karibu na chanzo hicho. Kwa kufanya hivyo, maji yanapatikana wakati wote kwani chanzo hakiathiriwi kwa namna yoyote.
Mradi huo wa maji umekuwa ni mkombozi kwa wakazi wa Heru Juu kwani upatikanaji wa maji safi na salama umeondoa magonjwa ya mlipuko kama kipindupindu na homa ya matumbo, hivyo afya za wakazi hao zimeimarika.
Serikali imetumia jumla ya bilioni 1.1 kutekeleza mradi huo ambao ulikamilika Mwezi Agosti, 2018.
Mradi huo umeendana na Sera ya Maji ya Taifa ya 2012 inayowataka wananchi kulinda na kusimamia vyanzo vya maji na pia kuwezesha upatikanaji wa maji kwa umbali usiozidi mita 400. Mradi wa maji wa Heru Juu, Kasulu umewawezesha wakazi wa maeneo hayo kupata maji kati ya umbali wa mita 5 hadi 400.