Ualbino ni ukosefu au upungufu wa rangi asili mwilini ambayo huathiri rangi ya ngozi, macho na nywele. Ualbino upo duniani kote na hutokea katika jamii zote, weusi, weupe, na waasia. Aina kuu za ualbino ni ualbino wa macho, ngozi na nywele.
Upungufu huo wa rangi asili mwilini husababisha watu hawa kukumbwa na changamoto mbalimbali ikiwemo za uoni hafifi, ngozi kuathiriwa na mionzi ya jua pamoja na kuwa kwenye hatari ya kutengwa na jamii kwa sababu hali yao haifahamiki na unyanyapaa kuanzia kwenye ngazi ya familia.
Leo tupofikia kilele cha maadhimisho ya uelewa juu ya watu wenye ualbino duniani ambayo kitaifa yanafanyika mjini Morogoro na mgeni rasmi akiwa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan jamii inapaswa kubadili mtazamo juu ya watu wenye ualbino kwa kuwatunza, kuwalinda na kuwasaidia katika ustawi wao.
Akizungumza na wahariri wa vyombo vya habari hivi karibuni mjini Morogoro, Afisa Uragibishaji wa Taaasisi ya Under the Same Sun (UTSS), Seif Kondo anasema kuwa pamoja na changamoto nyingine zinazowakabili watu wenye ualbino, saratani ya ngozi imekuwa chanzo kikubwa cha vifo ambapo wengi hufa kwa ugonjwa wa saratani ya ngozi chini ya umri wa miaka 40, kwa vile mionzi ya jua huharibu ngozi zao na matibabu stahili hayapatikani kwa wakati.
Ili kukabiliana na changamoto hiyo Kondo anasema “watu wenye ualbino wanatakiwa kutumia mafuta kinga kuanzia SPF 30 (sun serum) kuendelea, ambayo wakati mwingine hayapatikani kirahisi, naamini kuwa ikiwa mafuta hayo na matibabu yatapatikana kwa wakati basi tutapunguza idadi ya vifo vya watu wenye ualbino”.
Aidha, jamii inatakiwa kusaidia ustawi wa watu wenye ualbino kwa kuwaepusha na vitu mbalimbali vinavyoweza kuwaondolea kujiamini kwa mfano walimu kuwafikiria zaidi wanafunzi wenye ualbino kwa kuwaongezea muda wakati wa mitihani, kutoandika mwandiko mshazali, na wanafunzi hao kukaa viti vya mbele wakati wa masomo darasani.
Ni vyema jamii ikafahamu ukweli na kuusambaza kuwa ualbino ni hali ya kimaumbile, haisambazwi wala kuambukiza na hivyo mitazamo hasi kuwa ni makosa ya mama, watu hawa hawafi bali hupotea, chanzo cha utajiri, laana na kuwa ni watu wasio na thamani yoyote si mitazamo ya kweli, haina msingi wowote na inapaswa kupuuzwa.
Katika kuangazia hali ya watu wenye ualbino, mwandishi wa makala hii anadhani kuwa Serikali nayo ina mchango mkubwa katika kuboresha maisha na ustawi wao kwa kutengeneza sera, kutunga sheria na kuridhia mikataba inayowalinda.
Kama ambavyo tunafahamu kuwa katika miaka ya 2006, 2007, 2008 na mpaka 2015 yalitokea matukio kadhaa ya kukatwa viungo na hatimaye kuuliwa kwa watu wenye ualbino, ambapo Serikali ilichukua hatua za makusudi za kunusuru maisha ya watu hao kwa kwa kusitisha na kupitia upya vibali vya waganga wa jadi, pamoja na kuwakusanya watu wenye ualbino, hususani kwenye mikoa ya kanda ya Ziwa na kuwahifadhi kwenye baadhi ya shule maalum za Serikali kwa ajili ya usalama wao.
Baadhi ya shule hizo ni pamoja na shule ya msingi Mitindo iliyopo jijini Mwanza, Buhangija iliyopo mkoani Shinyanga, na Kabanga ya mkoani Kigoma.
Jitihada nyingine ya Serikali ni pamoja na kutungwa kwa Sheria ya Watu Wenye Ulemavu ya mwaka 2010, ikiwemo watu wenye ualbino ambayo inatoa mwongozo kwa ujenzi wa majengo yote na miundombinu kuzingatia hali za watu wenye ulemavu mbalimbali kwa kuwawezesha watu hao kutumia majengo hayo bila kadhia.
Sheria ya Ajira kifungu namba 31, nayo inatetea ustawi wa watu wenye ualbino ambayo inamtaka mwajiri wa sekta ya umma au binafsi atakayeajiri zaidi ya wafanyakazi 20 basi asilimia 3 ya wafanyakazi wake wawe watu wenye ulemavu wakiwemo wenye ualbino, ambao wana vigezo vya kufanya kazi hiyo.
Aidha, Sheria ya Ajira na Mahusiano Kazini ya mwaka 2004, kifungu cha 7 na kifungu kidogo cha 4 kinamtaka mwajiri kutoonesha vitendo vya kibaguzi kwa mwajiriwa mwenye ulemavu na ni kosa la jinai kumbagua mfanyakazi katika eneo la kazi.
Kama tunavyofahamu kuwa ni jukumu la kila Serikali duniani kulinda maisha na ustawi wa watu wake bila kubagua mtu yeyote, nayo Serikali ya Jamhuri ya Muungano imeendelea kufanya hivyo, kwa mfano katika Sheria ya Mtoto inakataza kwa mtoto mweye ulemavu kubaguliwa, sambamba na Sheria ya Taifa ya Uchaguzi ya mwaka 2010 ambayo inatoa ulinzi kwa watu wenye ulemavu.
Ni dhahiri kuwa Serikali imeendelea kutimiza wajibu wa kulinda wananchi hasa wenye ulemavu wakiwemo wenye ualbino, licha ya kuwa baadhi ya sheria hizo zimeendelea kutoa mwanya wa kuendeleza vitendo vya unyanywasaji kwa watu wenye ulemavu nchini.
Aidha, akizungumza kwa simu na mwandishi wa makala hii, kutoka mkoani Morogoro Mwanasheria wa Taasisi ya UTSS, Maduhu William anasema kuwa licha ya Serikali kuwa na Sheria za kusaidia ustawi wa watu wenye ulemavu nchini, bado kumekuwepo na changamoto mbalimbali kwenye utekelezaji wa sheria hizo.
William anasema, “Mfano Sheria ya Ajira kifungu namba 31, ni sheria nzuri na ambayo inatoa adhabu kwa mwajiri aliyekiuka kwa kutoajiri watu wenye ulemavu ambao pia wana vigezo kwa asilimia 3, kwa kutozwa faini ya milioni 2 au kwenda jela kwa muda wa miaka miwili au vyote kwa pamoja, hii tafsiri yake ni kuwa endapo mwajiri ana mtaji mkubwa wa bilioni kadhaa anaweza kukiuka sheria hii na endapo atashtakiwa basi atamudu kutoa faini kwa wepesi kwa vile ana uwezo mkubwa”
William anaongeza kuwa sheria inampa mamlaka waziri mwenye dhamana ya masuala ya watu wenye ulemavu kwa kutunga kanuni zinazoweza kusaidia ustawi wa jamii za watu hao, hata hivyo bado hatujawa na kanuni zilizotungwa kwa muktadha huo.
Masuala ya watu wenye ulemavu ikiwemo wenye ualbino ni jukumu la kila mtanzania, kwa vile watu hawa ni ndugu zetu, wazazi wetu, watoto wetu, jamaa zetu na marafiki zote na hivyo jamii yote ina jukumu la kumtunza na kumlea mtu mwenye ualbino ili aweze kufikia ndoto zake.
Ni wazi kuwa ndugu zetu hawa tunao kuanzia ngazi za familia, vijiji, mitaa au halmshauri zetu ni dhahiri kuwa tunao wajibu na jukumu la kuwalinda dhidi ya madhila mbalimbali hata kabla ya kusubiri Taasisi ya Ustawi wa Jamii kufikia katika maeneo yetu. Kwa kufanya hivyo tutakuwa tumeokoa maisha ya ndugu zetu, na kama tunavyofahamu kuwa Taasisi hii ya Ustawi wa Jamii nayo inakabiliwa na changamoto za vifaa kama magari, uhaba wa fedha na wataalamu na hivyo kushindwa kuhudumia watu wote kila mara wanapohitaji msaada.
Katika maadhimisho ya mwaka huu ya uelewa juu ya watu wenye ualbino duniani, ni rai yangu na imani yangu kwamba watanzania watafungua fikra mpya na kujua ukweli kwamba ualbino ni hali adimu kama ambavyo inasemekana kuwa nchini Tanzania, katika watu 1,500 mtu mmoja pekee ndio anaweza kuwa na uasili wa ualbino.
Ni dhahiri kuwa jamii inatakiwa kulinda thamani na utu wa watu wenye ualbino kwa vile ni sehemu ya jamii, inayohitaji upendo, kuthaminiwa na kulindwa dhidi ya madhila ya kimaumbile na mitazamo hasi ya kijamii.