Serikali imewaonya wanaofanya biashara ya upatu (Pyramid Scheme) kwa kuwa sio halali na hakuna taasisi wala mtu binafsi aliyepewa leseni ya kufanya biashara hiyo.
Onyo hilo limetolewa bungeni jijini Dodoma na Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji, wakati akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalum Mhe. Munira Mustafa Khatib, aliyetaka kujua ni lini Serikali itadhibiti biashara za upatu ambazo zimekuwa na athari kubwa kwa uchumi wa Taifa.
Dkt. Kijaji alisema kuwa, kwa mujibu wa sheria ya makosa ya jinai, biashara ya upatu ni haramu na huendeshwa kinyume na sheria na taratibu za nchi hivyo Serikali huchukua hatua dhidi ya wahusika kama ilivyofanya kwa taasisi ya DECI.
“Washiriki wa biashara ya upatu na wale wanaoshawishi ufanyaji wa biashara hiyo, wote wanatenda kosa na wanatakiwa kupata adhabu na sio kusaidiwa na Serikali”, alieleza Dkt. Kijaji.
Alisema kuwa Serikali itaendelea kutoa elimu kwa umma kuhusu madhara ya biashara ya upatu na tayari Benki Kuu ya Tanzania (BoT) kwa kushirikiana na na Mamlaka ya Masoko ya Mitaji na Dhamana (CMSA), ilitoa taarifa kwa umma kuhusu madhara hayo na kuwahimiza wananchi kutoa taarifa ya watu au taasisi inayofanya biashara hiyo.
Dkt. Kijaji alisema kuwa, kwa kuwa waathirika wakubwa wa biashara hiyo ni vijana na wanawake, Serikali kupitia Bunge, mwaka 2018, ilipitisha mabadiliko ya sheria ya fedha ambapo asilimia kumi ya mapato ya ndani ya halmashauri yanatakiwa kutolewa kama mikopo isiyo na riba kwa kundi hilo.
Alisema Wizara ya Fedha na Mipango kuna Taasisi ya huduma ndogo ya fedha-SELF, ambayo inatoa mikopo kwa kundi hilo kwa riba nafuu na inafanya vizuri katika maeneo mengi nchini.
Amewataka Vijana na wanawake kutojihusisha na biashara haramu bali watumie taasisi halali zinazotoa riba nafuu na zenye lengo la kujenga uchumi wa Taifa.