Mkuu wa Mko wa Dkt. Binilith Mahenge akiongea na wananchi wa Mtaa wa Chemchem kata ya Kingale alipofanya ziara ya kusikiliza kero za wananchi Kondoa Mji.
Mkuu wa Wilaya ya Kondoa Mhe. Sezaria Makota akiongea mbele ya Mkuu wa Mkoa wa Dodoma wakati wa Mkutano wa hadhara mtaa wa Chemchem kata ya Kingale.
Baadhi ya wananchi wa Mtaa wa Chemchem wakimsikiliza Mkuu wa Mkoa (Hayupo pichani) wakati wa ziara yake katika mtaa huo.
…………….
Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Dkt. Binilith Mahenge ameahidi kumaliza mgogoro wa Mtaa wa Chemchem na Gereza la King’ang’a ndani ya mwezi mmoja ili wananchi waendelee na shughuli zao za maendeleo.
Aliyasema hayo wakati wa mkutano wa hadhara uliofanyika katika eneo la Kambi ya Moto kata ya Kingale wakati wa ziara yake ya kusikiliza kero za wananchi iliyofanyika katika Halmashauri ya Mji Kondoa tarehe 12/06/2019.
“Ipo kazi iliyofanywa na Jeshi la Magereza na watalaam wa ofisi ya Mkuu wa Mkoa na ripoti ipo tayari nimeipata ila nikaona ni vyema nije kwanza kuwaona na kuwasikiliza wananchi kuliko kusoma tu taarifa ndio maana nimekuja leo naomba muongee kwa uwazi.” Alisema Dkt. Mahenge
Aidha aliwataka askari wa gereza la King’ang’a kuacha tabia ya kuwanyanyasa na kulisha mifugo yao katika mashamba ya wananchi kwani si busara kufanya hivyo na ni dhambi kubwa mbele ya Mwenyezi Mungu.
Aliendelea kueleza kuwa gereza ni la watanzania na ardhi ni ya watanzania hivyo hakuna haja kwa pande zote mbili kugombania fito ikiwa wote wanajenga nyumba moja ya Tanzania.
“Naomba mturuhusu tukalifanyie kazi suala hili ili tuje na majibu kamili ila nawasihi wananchi mkawe wavumilivu na msilete vurugu za aina yoyote katika kipindi hiki tutakuja kutoa majibu na viongozi wenu wote ili nao waendelee na kazi nyingine za kuwaletea maendeleo.” Alisisitiza Dkt. Mahenge
Hata hivyo aliwasihi wananchi na askari magereza kutoendeleza maeneo mapya yenye mgogoro kwa ajili ya kilimo na mifugo hadi hapo majibu yatakapotangazwa kwani tayari kila mtu eneo lake la awali alilokuwa akilifanyia kazi linajulikana.
Akiongea wakati wa mkutano Mkuu wa Wilaya ya Kondoa Mhe. Sezaria Makota alimuomba Mkuu wa Mkoa kumaliza suala hili mapema kabla ya msimu wa kilimo kuanza ili wananchi wanendelee na shughuli za kilimo.