‘Tunaomba WMO iweke miongozo maalumu ya usawa wa jinsi katika utekelezaji wa majukumu ya utoaji huduma za hali ya hewa ili nchi wanachama waweze kuwa na utaratibu wa pamoja kwenye utekelezaji wake hususan kwa wanawake’ alisema Dkt. Agnes Kijazi.
Dkt. Agnes Kijazi ambaye ni Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) na mwakilishi wa kudumu wa Tanzania katika Shirika la Hali ya Hewa Duniani (WMO) ambaye kwa sasa anagombe nafasi ya umakamu wa tatu wa Rais wa WMO alisema hayo wakati akichangia mjadala wa usawa wa jinsia (Implementation of WMO Gender Equality Policy and Action Plan ) kwenye mkutano wa 18 wa WMO unaoendelea jijini Geneva, Uswisi.
Vilevile, Dkt. Kijazi alielezea namna Tanzania kupitia TMA inavyoendelea kupiga hatua kuhakikisha usawa wa jinsia unazingatiwa kwa wanawake wenye utaalamu wa sayansi ya hali ya hewa kwa kuongezewa ujuzi (mafunzo), kushiriki katika kutoa utaalamu katika kamati za kikanda na kimataifa hasa suala la ushiriki wao katika makongamano na warsha mbalimbali.
Aliongezea kwa kusema, TMA imeweka miongozo mbalimbali ya kuwawezesha wanawake wenye sifa kupata nafasi za uongozi, hivyo kusaidia kuonesha uwezo wa wanawake katika utekelezaji wa majukumu wanayopatiwa. sambamba na kupata fursa ya kupaza sauti juu ya umuhimu wa usawa wa jinsia kwa kuwa mfano kwa taasisi za hali ya hewa Afrika na duniani kwa ujumla.
Dkt. Kijazi alitoa mfano wa ushiriki wa wanawake wa TMA katika Mkutano wa 50 wa Kikanda wa Nchi za Pembe ya Afrika (GHACOF-50) unaokusanya wadau kutoka nchi 10 za Pembe ya Afrika ili kuandaa utabiri wa msimu uliofanyika Rwanda ambao ulienda sambamba na kongamano lililohusu utoaji wa huduma za hali ya hewa zinazolenga mahitaji maalumu ya wanawake.
Tanzania ilipongezwa kwa kubadilishana uzoefu na nchi zingine wanachama wa Shirika la Hali ya Hewa Duniani kwa kuonesha jitihada zake za kusimamia usawa wa jinsia