Naibu Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Taifa Muhimbili- Mloganzila Dkt. Julieth
Magandi (wapili kutoka kulia) akizungumzia kuhusu matibabu na huduma ambazo
amepatiwa mtoto Hilary Plasidius ambaye alilazwa hospitalini kwa siku 210 na
kuruhusiwa leo. Anayemfuatia kushoto ni Daktari Bingwa wa watoto Mwanaidi Amir.
Daktari Bingwa wa watoto kutoka Hospitali ya Mloganzila Dkt. Mwanaidi Amiri akielezea kuhusu gonjwa uliokuwa ukimsumbua mtoto Hilary.
Dkt. Julieth Magandi (kulia) akizungumza mara baada ya kukabidhi msaada wa kiti
cha kumuwezesha kutembea mtoto Hillary, ambacho kimegharimu zaidi ya shilingi laki nne.
Mtoto Hilary akiwa mwenye tabasamu mara baada ya kuruhusiwa kutoka hospitalini
hii leo.
Bi. Patricia Hillary (katikati) akitoa neno la shukrani kwa wauguzi, madaktari pamoja na uongozi wa hospitali kwa kwa kumpatia matibabu mjuu kuu wake na afya yake kuimarika.
************************************
Dar es salaam 12-06-2019
Mtoto Hillary Plasidius mwenye umri wa miaka 8 aliyelazwa Hospitali ya Taifa
Muhimbili -Mloganzila kwa muda wa miezi minane na wiki mbili aruhusiwa huku
hospitali ikimsamehe gharama za matibabu na kumpatia msaada wa kiti mwendo
(wheelchair).
Mtoto Hillary alifikishwa Hospitali ya Mloganzila Oktoba 29 mwaka jana akiwa katika hali mbaya baada ya kuugua ugonjwa wa kupooza ambapo amekaa katika chumba cha wagonjwa mahututi (ICU) kwa siku 130 na wodini siku 124.
Daktari Bingwa wa watoto Dkt. Mwanaidi Amir amesema mtoto Hillary alipooza kuanzia miguuni mpaka shingoni hali iliyosababisha kupata shida ya kupumua na kushindwa kumeza na hatimaye kupoteza fahamu.
“Ugonjwa huu ulianzia miguuni mpaka shingoni ulienda kwa haraka sana na kusababisha ashindwe kupumua na kulazimika kumuweka katika uangalizi maalum, amekaa hospitalini kwa muda wa miezi minane tunafurahi kuona leo anaruhusiwa huku afya yake ikiendelea kuimarika’’amesema Dkt. Mwanaidi.
Kwa mujibu wa Dkt. Mwanaidi ugonjwa huu huwapata watu wazima na watoto ingawa hauna sababu lakini unatokea pale ambapo mtu amepata maambukizi ya kifua, maambukizi kwenye mfumo wa hewa au mfumo wa chakula ambayo yanaweza kuwa maambuki ya bakteria au virusi na kwamba mtu anaweza kupata dalili za ugonjwa baada ya wiki mbili baada ya kupata maambukizi.
Hivyo kinachotokea mwili unashambulia mishipa ya fahamu na kusababisha misuli kukosa nguvu na mara nyingi inaanzia miguuni kupanda mpaka juu.
Kwa upande wake Naibu Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Taifa Muhimbili-
Mloganzila Dkt. Julieth Magandi amesema Hospitali imetumia zaidi ya milioni 17 kugharamia matibabu ya mtoto Hillary. “Kumekuwa na dhana kwamba mgonjwa akiletwa Mloganzila gharama za matibabu ni kubwa suala ambalo si kweli kwani hakuna mgonjwa aliyepewa cheti akiambiwa kalete
dawa, lakini ieleweke kwamba kama huduma hazitachangiwa hazitakua endelevu na sisi lengo letu huduma hizi ziwe endelevu’’amesema Dkt. Magandi.
Amesema pamoja na kumptia msamaha wa matibabu, lakini Hospitali ya Mloganzila pia imempatia mtoto Hillary msaada wa kiti cha kumuwezesha kutembea ambacho kinagharimu zaidi ya shilingi laki nne.
Kwa upande wake bibi yake Hillary, ambaye anafahamika kwa jina la Patricia Hillary amewashukuru wauguzi, madaktari pamoja na uongozi wa hospitali kwa kuwezesha mjukuu wake kupata matibabu na afya yake kuimarika.